Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.George Waitara amewataka wadau na wataalamu wa michezo nchini kuja na mpango mahsusi wa namna nchi itakavyoweza kufikia katika kuendeleza sekta ya michezo nchini.
Akizungumza kwenye kikao cha maandalizi kwa ajili ya Mashindano ya Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari (UMISSETA) na Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) kilichoandaliwa na kampuni ya vinywaji ya Coca cola, Mheshimiwa Waitara amesema anatamani kuona walimu na wadau wengine waje na mpango mahsusi wa kuendeleza michezo ili Tanzania iondokane na tabia ya kuwa kichwa cha mwendawazimu katika sekta hiyo.
Mhe.Waitara amesema wataalamu waje na hoja ya kuendeleza sekta na michezo na anaamini kuwa walimu katika hili wana mchango mkubwa katika kuendeleza sekta ya michezo.
Amesema kwa kuwa watanzania wanapenda sana michezo, hakuna sababu ya kuwasononesha na badala yake akataka wataalam wa michezo kuja na mpango kabambe wa kukwamua sekta hiyo.
Mhe.waitara amesema pamoja na mchango mkubwa unaofanywa na walimu nchini katika kuinua maendeleo ya elimu nchini ambapo kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo kiwango cha ufaulu kimekuwa kikiongezeka, bado anaamini walimu wana jukumu kubwa katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanafundishwa michezo kwa nadharia na vitendo.
“ Natoa maelekezo kwa walimu wote kuhakikisha kuwa somo la michezo linafundishwa kwa nadharia na vitendo kama mtaala wa elimu unavyoelekeza,” amesema na kuongeza:
“ viwanja vya michezo vifufuliwe na vifanye kazi kama ilivyokusudiwa, viwanja vilivyovamiwa vipimwe na kuwekewa mipaka,” amesema.
Akizungumzia kuhusu maandalizi ya michezo ya umiseta na udhamini kutoka kampuni ya Coca cola, Naibu Waziri ameishukuru kampuni hiyo kwa kuendelea kudhamini mashindano hayo ambayo yamepangwa kufanyika kitaifa mkoani Mtwara kuanzia mwezi juni mwaka huu.
Pia Mhe.Waitara ameipongeza coca cola kwa kuanzisha shindano maalum la kutafuta shule bora zinazoongoza kwa kutunza na kuhifadhi mazingira ambapo mtoto ambaye atafanikiwa kuokota chupa kilo 600 na kuendelea watapata zawadi mbalimbali zikiwemo laptop.
Naibu Waziri amewataka Coca cola kuhakikisha kuwa shindano hilo linazifikia shule nyingi iwezekanavyo na ikibidi lifanyike kwa mikoa yote 26 nchini.
Mhe.Waitara amewaagiza Maafisa Elimu wa Mikoa, na Maafisa Elimu wa Wilaya kuhakikisha kuwa zawadi zote zitakazotolewa na kampuni hiyo zinagawiwa kwa walimu watakaoshinda na wanafunzi pia.
Wakati huo huo Naibu Waziri Waitara amewataka Maafisa elimu nchini kuhakikisha kuwa wanawasimamia walimu na wanafunzi ili waweze kupanda miti ya kutosha nchini ili waweze kukabiliana na athari za jangwa.
“Tukitaka kusaidia kampeni ya usafi wa mazingira hatuna budi kuanza na walimu na wanafunzi, tuhakikishe kila mwalimu shuleni anapanda mti mmoja na kila mwanafunzi anapanda miti miwili mmoja nyumbani na mwingine shuleni,” amesema.
Mapema Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Elimu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa bwana Julius Nestory ameipongeza kampuni ya vinywaji ya Coca cola kwa kuendelea kudhamini mashindano ya UMISSETA ambapo mwaka huu kampuni hiyo imeongeza kipengele cha usafi wa mazingira.
Amewataka maafisa elimu kuhakikisha kuwa zawadi zote zitakazonunuliwa na wadhamini coca cola zinawafikia walengwa na kwamba zawadi na jezi hizo kamwe zisiishie mitaani kwa wasiohusika.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.