Serikali imewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya matumizi ya fedha za serikali ili kupunguza matumizi mabaya ya fedha za serikali zinazotolewa kwa ajili ya Elimu.
Akifunga mafunzo elekezi kuhusu utekelezaji wa mradi wa lipa kulingana na matokeo katika Sekta ya Elimu (EP4R) jana jijini Dodoma, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Afya) Mhe. Josephat Sinkamba Kandege alisema kuwa serikali itahakikisha kuwa hakuna shilingi hata moja itakayopotea wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuhakikisha kuwa fedha yote itakayotolewa kwa ajili ya miradi inayopelekwa halmashauri ama iwe imetoka serikalini au kwa wahisani haitumiki kinyume na malengo yaliyokusudiwa
“Kila shilingi tunataka iwe na tija, hivyo nawataka wakurugenzi wa halmashauri na watendaji wengine mhakikishe kuwa mnafuata miongozo ili muepuke hoja za ukaguzi,” alisema
Aliongeza kuwa kila kiongozi anatakiwa kufanya kazi kwa weledi na kuacha tabia ya kufanyakazi kwa mazoea na kuzingatia miongozo na maelekezo ya matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo ili kuepuka hoja za wakaguzi.
Pia aliwaagiza watendaji hao kusimamia na kufatilia utekelezaji wa miradi hasa ujenzi wa miundombinu ya shule ili ikamilike kwa wakati na kuwashirikisha kamati, bodi na jamii inayozuguka katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupunguza ghalama zisizoza msingi, kutoa ajira kwa jamii husika na kuharakisha katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Alisema matumizi ya fedha yanayotumika katika miradi husika yaendane na thamani ya mradi husika ili kuhakikisha sekta ya elimu inapata matokeo chanya.
Aidha Mhe. Kandege alisema ili kuthibiti ubora wa elimu nchini halmashauri zihakikishe shule zinakaguliwa kwa wakati muafaka na changamoto zinazobainishwa na wathibiti ubora zifanyiwe kazi haraka ili watoto wa kitanzania wapate elimu bora.
“Wakaguzi wa Halmashauri toeni ushirikiano kwa wathibiti Ubora wa Elimu na Mafunzo elekezi kwa wakuu wa shule juu ya umuhimu wa kutekeleza ukaguzi wa ndani ya shule pale panapo kuwa na changamoto mawasiliano yafanyike kwa wakati kupitia Ofisi ya Mkoa ili muweze kufikia malengo ya pamoja,” alisema.
Mapema kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri kufunga kikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Elimu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Elimu ya Msingi Dkt. George Jidamva alisema changamoto kubwa waliyoiona kwenye utekelezaji wa mradi huo ni kwa baadhi ya watendaji kushindwa kujibu hoja za ukaguzi kwa kukosa vielelezo muhimu kama risiti na orodha ya malipo.
Changamoto nyingine ni kutofautiana kwa ubora wa majengo kati ya halmashauri na halmashauri licha ya kuwa ramani za miundombinu hiyo kufanana na hivyo kukosekana kwa thamani ya ubora kutokana na baadhi ya majengo kujengwa chini ya kiwango.
Mradi lipa kulingana na matokeo katika sekta ya elimu ( EP4R) ulianza Septemba, 2014 kwenye Mamlaka za serikali za mitaa kwa kupokea kiasi cha shilling bilioni 77.98 na kwa sasa halmashauri hizo zinatarajia kupokea kiasi cha shilling biloni 40 kutoka kwa wadau wa maendeleo ambazo zitatumika kwa mujibu wa maelekezo yatakayo tolewa na mamlaka husika.
Na: Majid Abdulkarim na Mathew Kwembe
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.