MKUU wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti ameitaka Idara ya Ardhi ya halmashauri ya mji wa Babati mkoani hapa kunyang'anya viwanja vyote vilivyoshindikana kuendelezwa ndani ya miaka mitatu.
Mnyeti aliyasema hayo jana katika kikao cha Baraza la Madiwani la kujibu hoja za mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) ambapo halmshauri hiyo imepata hati safi.
Mnyeti alisema wale wote wanaodaiwa hela ya viwanja na wameshindwa kuvilipia ndani ya miaka mitatu ikiwa ni pamoja na kushindwa kuviendeleza wanatakiwa wanyang'anywe na kuuziwa watu wengine wenye uhitaji wa viwanja.
"Sasa tukubaliane kwamba wale wote wanaodaiwa kutokana na mauzo ya viwanja wanyang'anywe na wauziwe watu wengine wenye uwezo wa kulipa vinginevyo hii hoja mwakani isijirudie.
"Kwa taarifa nilizonazo hivi viwanja vingi mmevinunua ninyi na hamtaki kulipa, Ofisa Ardhi pitia majina yote ya watu wanaodaiwa waite waambie mnalipia au hamlipii, na kama hamlipii chukua viwanja vyote tangaza watu wanunue na weka muda fulani hujalipa, kiwanja kinauzwa", Alisema Mnyeti.
Naye Diwani wa viti maalumu Praxidia Claud (Chadema) alimuomba Mnyeti kuingilia kati suala hilo kwani wao kama madiwani wanateseka na jambo hilo hali inayopelekea kulalamika kwamba halmashauri inakosa mapato.
“Mkuu wa mkoa hili ni jipu ambalo linatutesa sana katika halmshauri yetu, mara nyingi tumekuwa tukilalamika sana kwamba halmashauri yetu inakosa mapato, tunashindwa kuwalipa walinzi, tunashindwa kulipa maji, umeme.
“Haiwezekani toka viwanja vimetangazwa mtu kachukua zaidi ya miaka mitatu hajalipia na sisi tunashida na hela hatuna hata pesa ya kuwalipa vibarua wanaotufanyia usafi, kwa dhamira ya dhati Mh.mkuu wa mkoa tunaomba ushikilie hili”, Alisema Claud.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmshauri ya mji wa Babati, Yona Wawo (CCM) alisema toka mwaka 2014 walijiwekea malengo ya kupata fedha nyingi si chini ya Bil. 10 kutokana na mauzo ya viwanja.
“Sasa sababu zilizojitokeza ninatambua kwamba idara yetu ya upande wa ardhi haikufanya vizuri sana watu amepewa viwanja na wengine wana viwanja vingi sana na walichukua kienyeji hawajaweza kuvilipia vyote na imechukua muda wa miaka minne au mitano na hatupati fedha kwa halmashauri.
“Mimi kama Mwenyekiti wa halmashauri kwa sasa, nitahakikisha kwamba viwanja vyote ambavyo havijalipiwa tunavichukua kwa halmashauri tayari tunatangaza upya na tunaweka bei inayoendana na wakati”, Alisema Wawo.
(Kwa picha mbalimbali angalia sehemu ya Kituo cha Habari kisha nenda Maktaba ya Picha)
Imeandikwa na:Haji A.Msovu
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.