Mkurugenzi wa Huduma za afya, lishe na ustawi wa jamii Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt Ntuli Kapologwe amewataka waganga wakuu wa Mikoa na Halmashauri nchini kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujiunga na mfuko wa bima ya afya iliyoboreshwa.
Dkt. Kopologwe ametoa wito huo jana wakati akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake juu ya uhamasishaji wa jamii kujiunga na mfuko wa bima ya afya ilioboreshwa (CHF) ili kupunguza gharama zisizo za lazima wakati wa kupata huduma za afya kwa wananchi.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo Dkt. Kapologwe ameeleza kuwa asilimia 86 ya wananchi hawajajiunga na Bima ya afya nchini kutokana na kutopata elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa kuwa na bima ya afya ya jamii.
“Umuhimu wa kujiunga na bima ya afya ya jamii ni kuepuka gharama za matibabu za hapo kwa hapo katika hospitali,vituo vya Afya na zahanati zetu zilizopo nchini.
Pia amesema kuwa faida ya CHF iliyoboreshwa ni kuwa imeongeza wigo mpana wa upatikanaji wa huduma kwani ukiwa na hiyo bima popote pale ulipo nchini unaweza kupatiwa huduma za afya tofauti na awali huduma ilikuwa katika eneo ulilojiandikisha.
Hivyo taratibu za kujiunga na bima hiyo mwananchi anakwenda kujiandikisha katika ofisi za mitaa, vijiji, vitongoji na mawakala walio katika maeneo yao ili kuweza kusaidia wananchi kujiunga bila vikwazo.
“Baada ya maboresho kuna mfumo ambao unawezesha kutambua mtu wapi alisajiliwa na wapi ametibiwa na kurahisisha urejeshaji wa fedha katika kituo cha kutolea huduma husika”, ameeleza Mkurugenzi huyo.
Vile vile amesema kuwa bima ya afya iliyoboreshwa imepanua wigo wa mafao kwa kuongeza baadhi ya huduma kupatikana katika bima hiyo kama upasuaji mkubwa na mdogo.
Hivyo takribani vituo 6,000 vinauwezo wa kuwahudumia wananchi wanaojiunga na CHF iliyoboreshwa ikiwemo Zahanati 4,922, Vituo vya Afya 716, Hospitali za Wilaya 179 na Hospitali za Mikoa 28.
Aidha Dr. Ntuli aliongeza kuwa kwa upande wa ada kulifanyika utafiti kuweza kujua ni kiasi gani mwananchi anaweza kumudu ili aweze kuchangia ambapo asilimia 98 walisema wana uwezo wa kuchangia shilingi 30,000 ambapo ndicho kiasi kinachotumiwa kwa kila kaya moja ya watu wapatao sita kwa mwaka mmoja.
“Ada hiyo ni kwa maeneo yote isipokuwa Mkoa wa Dar es Salaam ambao ada yao ni shilingi laki moja na nusu kwa kaya moja yenye idadi ya watu sita na shilingi elfu arobaini kwa mtu mmoja na hii ni kutokana na wigo wa vituo vya kutolea huduma katika Mkoa huo ambapo vituo binafsi vitashirikishwa katika utoaji wa huduma ”,amesisitiza .
Pia amesema kuwa mwananchi akiwa amechangia kiasi hicho kwa mwaka na Serikali inachangia kiasi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa mwananchi.
Dkt.Kapologwe ameeleza kuwa tayari Serikali imechangia ruzuku ili kuhakikisha inaboresha huduma za mfuko wa bima ya afya ya jamii.
Mchango wa Serikali katika kuboresha huduma za afya imeboresha miundombinu kwa kujenga hospitali za wilaya mpya 102, vituo vya afya 487, zahanati 1198, ununuzi wa vifaa tiba kwa lengo la kuhakikisha huduma bora zinatolewa ili kutimiza matakwa ya wananchi.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.