Imeandikwa na: Mariamu Juma, Manyara
Watendaji katika ngazi za Mkoa na Wilaya wametakiwa kushiriana kwa karibu na maafisa ushirika na viongozi wa vyama vya ushirika kwa ajili ya kusimamia utaratibu wa mazao na ununuzi wa mazao ya dengu na mbaazi kwa msimu wa 2020/2021 ili mazao hayo yaweze kukusanywa kupitia vyama vya ushirika na kuuzwa katika soko la bidhaa la Tanzania (TMX) ambapo wanunuzi watanunua kwa ushindani kwa utaratibu utakaowekwa.
Hayo yalielezwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Joseph Mkirikiti katika kikao kazi cha wadau wa zao la dengu na mbaazi kilicholenga kupitia na kujadili rasimu ya mwongozo wa mauzo ya zao la dengu na mbaazi kwa msimu wa 2020/2021.
Mkirikiti alieleza kuwa serikali ya awamu ya tano kupitia wizara ya kilimo imetoa maelekezo ya mfumo rasmi ya ununuzi wa zao la ufuta,choroko,dengu,mbaazi na soya pamoja na waraka wa Waziri wa kilimo Na 2 wa mwaka 2020 kuhusu mifumo ya ununuzi wa mazao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na vyama vya ushirika.
Alisema lengo kuu la serikali ni kusisitiza mfumo huo na kuhakikisha kuwa kilimo cha mazao husika kinamnufaisha mkulima hususani mkulima mdogo sambamba na kuthibiti mfumo holela wa ununuzi wa mazao hayo ambayo kimsingi ulikuwa haumnufaishi mkulima mdogo.
‘’Madhumuni ya kukutana hapa ni kushikishana katika kupitia mapendekezo ya muongozo wa utaratibu wa mauzo ya mazao ya dengu na mbaazi hapa mkoani kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kama utekelezaji wa maagizo ya serikali ambapo seerikali inataka mfumo huu utumike katika mauzo ya mazao husika ili kuhakikisha mkulima anapata soko la uhakika na lenye manufaa ambapo hii inalenga wadau wote wanaoshiriki katika mnyororo wa thamani wa mauzo ya zao husika’’alisema Mkirikiti.
Hata hivyo Mkirikiti alisema kuwa taarifa alizo nazo ni kuwa Mkoa wa Manyara tayari umeanza mfumo wa utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi za ghalani kwa msimu wa 2019/2020 kwa zao la ufuta kupitia vyama vya ushirika na soko la bidhaa Tanzania (TMX) ambapo matokeo chanya yamepatikana kwa mkulima kupata bei shindani ikilinganishwa na uuzaji holela ambapo pia ushuru wa halmashauri uliongezeka , vijana zaidi ya 100 walipata ajira na mama lishe .
Wakulima walieleza kuwa ili kuendana na mfumo huo ambao serikali imeuweka na walikiri kuukubali ni vyema serikali ikaangalia mfumo mzuri wa kumuwezesha mkulima anapokuwa na shida na mazao yake yatakapokuwa tayari akatwe fedha hizo kupitia mazao yake pindi yatakapouzwa.
‘’Tunataka serikali itusaidie pale tunapokuwa na shida wengine tunasomesha watoto inapotokea nadaiwa ada ili mwanangu aendelee na masomo halafu naomba kukopesha kupitia ushirika ili nikivuna mazao yangu muda wa kuuzwa nikatwe hiyo pesa unakuta haiwezekani hii inatusukuma sisi kwenda kwa madalali ambao mwisho wa siku wanatunyonya sana sasa kwa kuwa unashida inakubidi uchukue’’Jumanne Shabani ambaye ni mkulima.
Aidha Mkuu wa Mkoa huo akatoa wito kuwa mtu yeyote atakayegundulika anaenda vijijini kuwahamasisha wakulima kutokujiunga na mfumo wa stakabadhi ghalani watahakikisha wanamkamata.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.