Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameziagiza Wizara ya Ofisi ya Rais, Tamisemi na ile ya Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto kukutana na kupitia muundo wa utumishi kwa maafisa ustawi wa jami ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii wa Mikoa na Halmashauri unaofanyika kwa siku tatu kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete uliopo Jijini, Dodoma.
Wizara hizi mbili zikutane na kuangalia namna bora ya kubadili muundo wa maafisa hawa ili kuwatengenezea mazingira mazuri kwa ajili ya kazi yao.
“Maafisa Ustawi ni watu muhimu sana kwenye jamii ni muhimu nafasi yao iwekwe vizuri kwenye muundo na kama italazimu kubadili muundo ili kazi yao ifanyike vizuri mfanye hivyo na kama ni suala linalohitaji marakebisho ya sheria mlete na bahati nzuri hapa tuna mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe Jason ( Mb) litafanyiwa kazi” alisema Mhe Majaliwa.
Wakati huo huo Waziri Mkuu Majaliwa amekemea tabia ya halmashauri kuwataka watu wenye ulemavu kutoa asilimia 10 ya mkopo wanaochukua kama dhamana wakati wa kupewa mikopo.
“Kuna mbunge amesema kuna halmashauri zinawataka watu wenye ulemavu kutoa asilimi 10 ya thamani ya mkopo wanaochukua kama depost, jambo hilo haliwezekani.
Mhe. Majaliwa aliongeza: “ Kuwataka waweke depost hilo jambo halipo na hata Sheria yenyewe haisemi hivyo, hivi watu wenye ulemavu watazipata wapi fedha hizo?
“ Ninyi maafisa ustawi wa jamii hakikisheni mnalisimamia hilo, fedha inatakiwa kutolewa kama sheria inavyoruhusu, na hii si kwa mapenzi ya mkurugenzi au baraza la madiwani.
Serikali iliweka sheria ambayo inazitaka kisheria halmashauri zote nchini kutenga asilimia 10 kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya wanawake na vijana na asilimia 2 zinaelekezwa kwa watu wenye ulemavu, asilimia nne kwa wanawake na asilimia 4 kwa vijana.
Naye Naibu Waziri wa Tamisemi, Mhe. Josephat Kandege alisema Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuimarisha sekta ya ustawi wa jamii kwa kutekeleza matakwa ya kisheria yenye dhamira ya kuboresha ustawi wa jamii yetu hapa Nchini .
Alisema tumeandaa Waraka wa utekelezaji wa Sheria ya Wati wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 lengo ikiwa ni kuhimiza wajibu wa Wakuu wa Mikoa katika kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 9 ya watu wenye ulemavu.
Pia tumepeleka Waraka wa mwaka 2018 kwa Wakuu wa Mikoa kushughulikia mashauri ya watoto ili kupunguza ama kuzuia ukatili dhidi ya watoto alisema Kandege.
“Kwa nyakati tofauti bajeti ua utekelezaji wa masuala ya Ustawi wa Jamii umekua ukifungamanishwa pamoja na bajeti ya Lishe , kwa bajeti ya mwaka 2019/20 tumefanikiwa kufanya maboresho ya kimfumo ambapo Bajeti za Ustawi wa Jamii umewekewa dirisha maalumu ndani ya mfumo wa Planrep ambalo linajulikana kama “Council Comprehensive Social Welfare Operatiobal Plan”; Jitihada hizi zitasaidia kuongeza ufanisi katika uwajibikaji wa watendaji, kuweka uwazi na kudhibiti matumizi ya fedha za miradi ikiwemo fedha za wadau wa maendeleo” alisema Kandege.
Naye Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile aliwaagiza maafisa ustawi wa jamii nchi nzima kukaguza vituo vya kulelea watoto ili ambavyo havina sifa na vibali halali vifungwe.
“ Kumekuwa na ongezeko la vituo vya kulelewa watoto yatima, bahati nzuri kuna watu ambao ni waaminifu, lalini kuna wengine wasiowaadilifu, Tumepokea malalamiko kuwa baadhi ya watu wanawatumikisha watoto hao kwenye biashara ya ombaomba, biashara ya ngono na vingine kuwa vituo vya kususanyia watoto kwa ajili ya biashara ya utumwa.
“ Hivyo maafisa wote manatakiwa kuvikagua vituo hivi na visivyo na sifa vifungwe na hakikisheni wanawaletea taarifa zao kila robo mwaka, nusu mwaka na za mwaka mzima.”
Pia Dk. Ndungulile alisema serikali iko katika hatua ya kuandika sheria itakayosimamia sekta hiyo sambamba na uanzishwaji wa Baraza litakalosimamia maadili ya maafisa ustawi wa jamii.
Naye Mwakilishi wa Mkazi wa UNICEF, Maniza Zamani pamoja na kuishauri serikali kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji kazi kwa maafisa ustawi wa jamii na kuahidi kuwa wadau wa maendeleo nchini Tanzania wataendelea kuisaidia serikali katika kuimarisha sekta hiyo ili kuboresha utoaji wa huduma.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Rais Tamisemi, Rasheed Maftah alisema lengo la mkutano huo ni kukumbushana maadili ya kazi Lengo la kukumbushana maandili ya kazi, uwajibikaji na weledi katika kuhudumia wananchi wenye mahitaji.
“ Pia tumekutana ili kuepana mrejesho wa utekelezaji wa shughuli za ustawi wa jambii kwenye mamlaka za serikali za mitaa na kuwezesha kufahamu mafanikio na
“ Pia kujadili maendeleo na changamoto zinazohusu utoaji wa huduma za ustawi wa jamii katika mikoa na mamlaka za serikali za mitaa na kushirikishana mbinu za utatuzi na hatimaye kupeana uelekeo wa pamoja wa utekelezaji wa mwaka huu wa fedha 2019/2020.
Mkutano huu unaofanyika kwa mara ya kwanza toka majukumu ya ustawi wa jamii yagatuliwe mwaka 2006 unaenda sambamba na Kauli Mbiu “Uadilifu, Weledi na Uwajibikaji katika utoaji wa huduma za Ustawi wa Jamii Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni Nguzo katika kuelekeza uchumi wa kati wa viwanda”.
Na:TAMISEMI
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.