Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mh.Harrison G.Mwakyembe amefanya ziara ya siku mbili Mkoani Manyara kwa kuzindua warsha ya wadau wa filamu Mkoani Manyara, kutembelea viwanja vya Michezo na kutembelea vivutio vya kiutamaduni vilivyopo Mkoani Manyara.
Katika ziara hiyo Mh Waziri tarehe 10/07/2018 alifungua warsha ya wadau wa filamu iliyofanyika ukumbi uliopo Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Manyara, warsha iliyoandaliwa na Bodi ya filamu Tanzania, yalitotolewa na Wataalam kutoka Chuo Cha Sanaa cha Bagamoyo na kuhudhuriwa na wasanii mbalimbali wa Mkoani Manyara.
Mh. Waziri aliwataka wadau wa filamu kuzingatia mafunzo hayo ili waweze kuandaa filamu bora zenye ushindani katika soko kwani Tanzania ni nchi ya pili Afrika kwa utengenezaji wa filamu baada ya Nigeria kwa hiyo kuna haja ya kuwa na watengenezaji filamu bora wenye weledi juu ya fani hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii Afisa Utamaduni wa Mkoa wa Manyara Bi.Frida alisema mafunzo hayo yatawasaidia wasanii wetu kujua mbinu mbalimbali za utengenezaji wa filamu na kuwataka wasanii hao kutembelea Ofisi za Utamaduni zilizopo katika kila Halmashauri za Mkoa huo ili kujiongezea uwezo mara wanapohitaji ushauri juu ya uandaaji wa filamu,pia wasanii hao wanaweza kutembelea Ofisi za Maafisa Habari na Mawasiliano ili kujifunza juu ya upigaji picha bora na uandishi sahii wa miongozo kwa madhumuni ya kuboresha filamu zao.
Baada ya ufunguzi wa warsha hiyo Mh. Waziri alitembelea viwanja vya michezo vilivyopo Shule ya Sekondari ya Singe,Shule ya Sekondari Ayalagala,Uwanja wa Kwaraa na Ofisi ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Manyara na kujionea jinsi Mkoa ulivyokuwa na viwanja bora katika michezo ya Mpira wa Pete,wavu na mpira wa kikapu, Pamoja na kuwa na viwanja bora katika michezo hiyo lakini Mh.Waziri alijionea changamoto zilizopo katika viwanja vya Mpira wa Miguu kwani Mkoa hauna viwanja vye hadhi kwa ajili ya mchezo huo, vilevile alishuhudia changamoto zilizopo katika mchezo wa riadha pamoja na Mkoa wa Manyara kuwa ni miongoni mwa mikoa inayozalisha wanariadha wengi nchini lakini Mkoa huo hauna hata chuo kwa ajili ya kufundishia wanariadha.
Mh. Waziri Mwakyembe alitoa ahadi ya kujenga chuo cha pili cha michezo cha Serikali mkoani Manyara baada ya kile cha Malya na kuwataka viongozi wa riadha Mkoani humo kutafuta wanariadha wasichana watano kwenda kwenye mashindano Mkoani Dar es slam ili wakashindanishwe na kupata nafasi ya kwenda Japan kujifunza juu ya mchezo wa riadha.
Pia alipata fursa ya kusaliamiana na walimu wa mchezo wa Pete waliopo kwenye mafunzo ya ualimu wa mchezo huo yaliyoandaliwa na Chama cha Mchezo wa pete Tanzania (CHANETA) yanayofanyika katika viwanja vya Kwaraa.
Vilevile alipata fursa ya kutembelea Ofisi ya Waandishi wa Habari Mkoani Manyara na kuwasifia sana kwa kuwa na Ofisi nzuri kwani mikoa mingi sana nchini haina ofisi za waandishi na kuwaahidi kuja kufanya Harambee ya kujenga ofisi ya kisasa.
Siku ya pili Mh. Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo alitembelea vivutio vya utalii wa kiutamaduni kwa kutembelea katika Kichuguu chenye Volkano tuli na Chemchem ya Maji ya moto ya asili vilivyopo Kitongoji cha Maji ya Moto Kijiji cha Masware kata ya Magugu Halmashauri ya Wilaya ya Babati na kuwataka wataalam kuvitangaza vivutio hivyo ili watu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kuweza kufanya utalii wa kiutamaduni katika maeneo hayo.
Ziara ya Waziri Habari ilihitimishwa kwa kutembelea Ziwa Babati lilipo Halmashauri ya Mji wa Babati na hatimaye kuongea na wadau mbalimbali wa wizira hiyo katika ukumbi wa White Rose kwa kusikiliza changamoto mbalimbali na kujibu maswali. Mheshiumiwa Waziri Mwakyembe aliahidi kuzitafutia utatuzi changamoto hizo.
(Kwa picha mbalimbali za matukio ya ziara hiyo angalia kwenye mkanda wa Bluu nenda Media Centre kisha nenda kwenye Maktaba ya picha)
Imeandikwa na: Haji A.Msovu(Afisa Habari Mkoa wa Manyara)
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.