Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa ametembelea Mkoani Manyara Wilaya ya Kiteto,ambapo alipata fursa ya kuongea na wananchi wa Kijiji cha Engusero,kupokea taarifa ya Mkoa na Wilaya, kuongea na Watumishi wa Umma, viongozi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali na Madiwani; kadhalika kutembelea Hospitali ya Wilaya; Kukagua na kuweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa jengo la Ofisi za Halmashauri ya Wilaya,pia kuongea na Wananchi katika Mkutano wa hadhara katika uwanja wa Jamhuri Mjini Kiteto.
Aidha Mheshimiwa Majaliwa aliwasalimia wananchi wa kijiji cha Engusero akiwa njiani kuelekea Kiteto, wananchi walilalamikia kero maji, Kituo cha Afya kutokuwa na chumba cha kuhifadhia maiti, Chumba cha upasuaji wodi ya wagonjwa,Gari ya wagonjwa kuchukuliwa na Halmashauri, na barabara ya lami kutoka Mbande (Kongwa) hadi Kibaya (Kiteto),pamoja na hayo,Wananchi hao walieleza wasiwasi wao mkubwa wa kukumbwa na njaa kutokana na kuwepo kwa viashiria vya ukame,vile vile waliomba kujengewa soko la kimataifa ili kuwezesha kuuza mazao yao bila kusafirisha.
Mheshimiwa Majaliwa aliagiza Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wafike katika eneo husika ili waangalie namna ya kutatua changamoto za Kituo cha Afya,pia viongozi wa halmashauri waende kufanya tathmini na kutoa mapendekezo ya Ujenzi wa soko hilo lililoombwa na wananchi wa Engusero.
Hata hivyo Mheshimiwa Majaliwa aliweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, akiwa katika eneo la mradi alipata fursa ya kukagua jengo hilo ikiwa ni pamoja na kuwapongeza Halmashauri kwa kubuni mradi huo, pia Mheshimiwa Majaliwa aliwataka wasimamie ujenzi huo na kulikamilisha jengo hilo kwa wakati ili thamani ya fedha ionekane, kwani jengo hilo ni kubwa na la kwanza ama la pili nchini baada ya Lushoto na Peramiho.
Mheshimiwa Majaliwa alipata fursa ya kuhutubia katika Mkutano wa Hadhara Uwanja wa Jamhuri Kiteto, akiwa katika mkutano huo alishuhudia maombi maalum yaliyofanywa na viongozi wa kidini na wazee wa kimila, jamii za Kinguu, Kigogo, Kimasai na Kikamba ambao waliunda kamati ya maridhiano na kukubaliana kuzika tofauti zilizowahi kujitokeza baina ya wakulima na wafugaji.
Aidha Mheshimiwa Majaliwa alikutana na changamoto ya maji,barabara,migogoro ya ardhi pamoja na kero za baadhi ya michango katika elimu na kuahidi kuendelea kuzitatua changamoto hizo kwa kutekeleza ilani ya CCM ili kuwaletea wananchi maendeleo na kutatua changamoto zinazowakabili.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.