Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara leo imepokea chupa sita zenye ujazo wa nusu lita kila moja za Vitendanishi kwa ajili ya kuangalia madini joto kwenye chumvi kutoka Taasisi ya Chakula na lishe Tanzania (Tanzania Food and Nutrition Centre - TFNC).
Akikabidhi vitendanishi hivyo Mchunguzi wa Maabara kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Bi.Aldegunda Marundu amesema kuwa wao kama Taasisi wameamua kuusaidia Mkoa wa Manyara ili kuweza kupima madini joto kwenye chumvi na hivyo kupunguza na kuondoa maradhi yaletwayo na ukosefu wa madini joto kwenye chumvi.
“ Vitendanishi hivi tumevipata kutoka kwa wafadhili wetu ambao ni TFNC na GAIN na hivyo kuamua kuvisambaza kwenye mikoa mbalimbali hususan Mikoa inayozalisha chumvi kama Manyara” Alisema Bi. Marandu.
Lengo la kufanya usambazaji wa vitendanishi hivyo ni kuwezesha kuendelea kwa zoezi la upimaji wa viwango vya madini jotokwenye chumvi ambao umekuwa ukifanywa na maabara ili kuhakiki viwango vya madini joto yaliyowekwa kwenye chumvi inayotumiwa na jamii. Kwa kufanya hivyo itasaidia kupunguza na hata kuondoa kabisa matatizo yatokanayo na upungufu wa madini joto.
Akipokea Vitendanishi hivyo kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Dkt. Pastory Mahendeka pamoja na kuwashukuru TFNC kwa msaada wao pia aliwaaomba wafadhili hao kuwezesha usimamizi shirikishi katika Mkoa wa Manyara wa kubaini uwepo wa madini joto kwenye chumvi ili kuziwezesha jamii za Mkoa wa Manyara kufahamu umuhimu wa kutumia chumvi yenye madini joto na pia kujua madhara yatokanayo na matumizi ya chumvi isiyo na madini joto.
“Napenda kuwashukuru wafadhili wetu kwa msaada wa vitendanishi hivi, kiukweli katika Mkoa wa Manyara vitendanishi vilituuishia na kwa kupata vitenganishi hivi vitasadia kuendelea na zoezi la upimaji wa madini joto kwenye chumvi” Alisema Dkt.Mahendeka.
Kulingana na Shirika la Afya duniani matumizi ya chumvi yenye madini joto katika ngazi ya kaya yanapaswa kuwa zaidi ya asilimia 90 ili kuwezesha kuondokana na madhara yatokanayo na upungufu wa madini joto. Asilimia 65 ya sampuli ya chumvi ya mawe kutoka katika maduka ya reja reja, sokoni na kwenye minada zimebainika kutokuwa na madini joto. Aidha, asilimia 25 ya sampuli za chumvi zilizofungashwa katika pakiti zilizokusanywa kutoka katika maduka ya rejareja hazikuwa na madini joto. Kuhusiana na sampuli za chumvi kutoka ‘supermarkets’, mchanganuo wa kimaabara unaonesha kuwa asilimia 54.6 ya chumvi hizo hazikuwa na madini joto.
changamoto zinazoukabili mpango wa kuchanganya madini joto katika chumvi ni pamoja na uelewa mdogo wa madhara ya upungufu wa madini joto kwa wadau na baadhi ya viongozi wa serikali wenye dhamana ya kutoa maamuzi, upatikanaji endelevu wa fedha na vitendea kazi (rapid salt test kits na vyombo vya usafiri) kwa ajili ya ukaguzi na ufuatiliaji, ukaguzi na uchukuaji wa sampuli za chumvi wa mara kwa mara hasa ukaguzi madhubuti kwa wazalishaji kabla ya chumvi kusambazwa, udhaifu katika utekelezaji wa sheria na kanuni, kukubalika kwa dhana ya matumizi ya chumvi yenye madini joto na uwepo wa wazalishaji wadogo wa chumvi wanaoingiza sokoni (kwa walaji) chumvi isiyo na madini joto.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.