Wilaya ya Mbulu ni miongoni mwa Wilaya tano (5) zinazounda Mkoa wa Manyara. Wilaya ya Mbulu ni Wilaya kongwe ilianzishwa sawa na Mji wa Nairobi 1905. Wilaya ya Mbulu imepakana na Wilaya ya Karatu kwa upande wa kaskazini, Wilaya ya Babati kwa upande wa mashariki, Wilaya ya Hanang' kwa upande wa kusini na Wilaya ya Mkalama kwa upande wa magharibi. Wilaya ya Mbulu ipo Kaskazini mwa Tanzania Bara na ipo kati ya Latitudo 3.0° na 4° 16' Kusini mwa Ikweta na Longitudo 35° na 36° Mashariki mwa Grinwich. Aidha, Wilaya ina ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 4,350.
Wilaya ina misimu miwili ya mvua ambapo mvua za vuli zinaanzia mwezi Novemba hadi Disemba na mvua za masika zinanyesha miezi ya Machi hadi Mei. Wastani wa mvua ni kati ya mm 600-1200 na wastani wa joto ni nyuzi sentigredi 18 ila kuna tofauti kwa miezi ya Februari/ Machi na Novemba/Disemba ambapo joto hufikia nyuzi sentigredi 20 hadi 21. Miezi ya baridi ni Juni na Julai, ambapo nyuzi joto hushuka hadi sentigredi 15.4
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012; Wilaya ya Mbulu ilikuwa na jumla ya wakazi 320,279 kati yao 161,548 ni wanaume na 158,731 ni wanawake. Pia Wilaya inakadiriwa kuwa na ongezeko la asilimia 3.8 ya idadi ya wakazi kila mwaka ikilinganishwa na ukuaji wa Taifa wa asilimia 2.9. Aidha, Wilaya ya Mbulu ina wastani wa watu 6 kwa kila kaya.
Wilaya ya Mbulu ina Halmashauri mbili. Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu iligawanywa mwaka 2015 na kuunda Halmashauri mbili ambazo ni Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na Halmashauri ya Mji wa Mbulu. Wilaya ya Mbulu ina jumla ya Tarafa 5, Kata 35, Vijiji 110, Vitongoji 515 na Mitaa 58 iliyoandikishwa. Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ina jumla ya Kata 18, Vijiji 76 na Vitongoji 362 na Halmashauri ya Mji wa Mbulu ina kata 17, Vijiji 34, Vitongoji 153 na Mitaa 58. Wilaya ina majimbo mawili ya uchaguzi yenye Jumla ya Madiwani 47, ambapo Jimbo la uchaguzi la Mbulu Vijijini lina Madiwani 24 kati yao Madiwani 18 ni wakuchaguliwa na 6 ni wa kuteuliwa (Viti Maalum) na Jimbo la uchaguzi la Mbulu Mjini lina Madiwani 23 kati yao Madiwani 17 ni wa kuchaguliwa na 6 ni kuteuliwa (Viti Maalum). Aidha katika Jimbo la Mbulu Vijijini kuna Mbunge 1 wa kuchaguliwa na Jimbo la Mbulu Mjini kuna Wabunge 2 ambapo 1 ni wa kuchaguliwa na Mbunge 1 ni wa kuteuliwa (Viti Maalum) wote wametokana na Chama cha Mapinduzi.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.