MKUU WA MKOA WA MANYARA AKABIDHIWA MAJIKO BANIFU 7,914 KWA BEI YA RUZUKU.
Na, Ruth Kyelula, Manyara RS
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe.Queen Sendiga, amekabidhiwa majiko banifu 7,914 kwa bei ya ruzuku ya shilingi 11,200 ambayo ni sawa na asilimia 80, ambapo kwa bei ya awali ya jiko illikua shilingi 56,000.


Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe.Queen Sendiga akikagua majiko banifu ya REA
Majiko hayo, alikabidhiwa Novemba 10, 2025, ofisini kwake Wilayani Babati kutoka kwa Wakala wa Nishati safi Vijijini (REA) ikiwa ni juhudi za Serikali kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia na kulinda mazingira.


Aidha Mhe. Sendiga, alisema kuwa mpango huo wa usambazaji wa majiko banifu utafanyika katika Wilaya zote tano za Mkoa wa Manyara na kuhakikisha wananchi wote wanapata, hususani wa kipato cha chini na wanapata fursa ya kutumia nishati safi na salama kwa bei nafuu.


“Nawaagiza, Wakuu wote wa Wilaya wa Mkoa wa Manyara, kusimamia kwa makini zoezi hili, ili kuhakikisha majiko hayo yanauzwa kwa bei iliyoelekezwa na kuepuka udanganyifu wa aina yoyote unaoweza kujitokeza wakati wa zoezi.” Alisema, Mhe.Sendiga.

Mhe. Sendiga, alisema kuwa, kampeni hii ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kupunguza uharibifu wa mazingira unaosababishwa na matumizi makubwa ya kuni na mkaa na pia kulinda afya za wananchi.

Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.