Na, Ruth Kyelula, Manyara RS
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Mhe. Dkt.Florence Samizi (Mb), ameagiza miradi iliyofikia asilimia 96 na 94 ikamilike mara moja na wananchi waanze kupata huduma mara moja hadi ifikapo Desemba 27, 2025.

Aliyasema hayo alipokua amefanya ziara ya kukagua miradi mitatu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara. Ziara hiyo aliifanya jana Novemba 26, 2025, akiambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Mganga Mkuu wa Mkoa,Mbunge wa Babati mjini pamoja na wadau wengine wa afya, ambapo walikagua ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharula (EMD),jengo la wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU) pamoja na jengo la Damu Salama.

“Nimetembelea miradi mitatu tuliyokuwa tumekusudia kuitembelea, ambapo ni jengo la dharula la wagonjwa, tumeliona lipo asilimia 94, lakini pia tumetembelea jengo la wagonjwa mahututi tumeona lipo asilimia 96, na tumetembelea jengo la damu salama ambalo tumeona lipo asilimia 75.Nichukue nafasi hii kuwapongeza kwa kazi nzuri ya kusimamia miradi hii mpaka imefika sehemu hii, Lakini sasa niwaombe Miradi iliyofika asilimia 96 na 94 kwa maana ya jengo la dharula na jengo la wagonjwa mahututi yamalizike haraka na yaanze kazi mara moja kama mlivyoahidi kwenye taarifa yenu.” Alisema Naibu Waziri, Mhe. Dkt. Florence.

Aidha Mhe. Florence ametoa wito kwa watumishi wa afya kufanya kazi kwa umoja, upendo na mshikamano huku wakiendelea kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa na kufanya kazi kwa moyo.

Kaimu Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Dkt. Yesige Mutajwaa
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Bi. Maryam Muhaji alisema kuwa watatekeleza maagizo hayo na kukamilisha majengo hayo kwa wakati.

Nae Kaimu Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Dkt. Yesige Mutajwaa, amesema kuwa ujenzi wa majengo hayo matatu upo hatua za mwisho kukamilika.Ambapo hadi kukamilika majengo hayo jumla ya fedha Bilioni tatu (3) zitatumika.

Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.