Bw.Nicodemu Bonifasi Tlaghasi (Nyeusi) wa Chama Cha Mapinduzi amewashinda wagombea wa CHADEMA Bw. Mathias Zebedayo Bombo na Bw. Issa Athumani Ally wa UPDP katika uchaguzi mdogo uliofanyika jana tarehe 12/08/2018 katika Kata ya Bagara Halmashauri ya Mji wa Babati Mkoani Manyara.
Akitangaza matokeo hayo mbele ya umati uliofurika katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mji Babati Msimamizi wa uchaguzi Bw.Fortunatus Fwema alisema waliojiandikisha walikuwa 16307 wapiga kura walikuwa 4246 sawa na asilimia 46 ya waliojiandikisha,kura zilizoharibika ni 38 sawa na asilimia 1,kura halali ni 4208 sawa na asilimia 99 ya kura zilizopigwa, Bw.Nicodemu Bonifasi Tlaghasi (Nyeusi) wa Chama Cha Mapinduzi kura 2708 sawa na asilimi 64 ya kura zilizopigwa, Bw. Mathias Zebedayo wa Chadema kura 1455 sawa na asilimia 34 ya kura zilizopigwa na Bw. Issa Athumani Ally wa UPDP alipata kura 83 sawa na asilimia 2 ya kura zilizopigwa.
Msimamizi wa uchaguzi huo alivishukuru vyama vilivyoshiriki, ambavyo havikushiriki uchaguzi na wananchi kwa ujumla kwani uchaguzi umefanyika kwa amani na utulivu na hakuna tukio lolote la uvunjifu wa amani lililoripotiwa tangu kufunguliwa kwa vituo saa moja asubuhi hadi saa kumi vituo vilipofungwa na kuanza kuhesabu kura na baadae majumuisho yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmasjhauri ya Mji Babati.
Uchaguzi huo umefanyika baada ya aliyekuwa Diwani wa Chadema kujiuzulu nafasi yake na kuhamia CCM.
(Kwa picha mbalimbali na video za Uchaguzi huo angalia sehemu ya Kituo cha Habari kisha nenda Maktaba ya Picha na Maktaba ya Video)
Imeandikwa na: Haji A.Msovu (Afisa Habari Mkoa wa Manyara)
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.