Na Nyeneu, P. R - Dongobesh
Kufuatia maelekezo ya serikali kuwa maadhimisho ya sherehe za Miaka 59 ya Muungano kwa mwaka huu zifanyike katika ngazi ya Mikoa nchini kote, Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Charles Makongoro Nyerere leo tarehe 25 Aprili, 2023 ameungana na viongozi mbalimbali wa Mkoa akiwemo Katibu Tawala wa Mkoa, Viongozi wa Ulinzi na Usalama wa Mkoa na wananchi wa Wilaya ya Mbulu kushiriki zoezi la Upandaji miti 154 kwenye eneo la Hospitali ya Wilaya ya Mbulu na eneo la jengo la utawala la Halmashauri Mjini Dongobesh miti 258 hivyo kufanya jumla ya miti 412.
Lengo la kuadhimisha maadhimisho katika ngazi ya mikoa ni kuwapa fursa wananchi kuelewa kwa undani maana ya Muungano ulioasisiwa na waasisi wetu. Katika Hafla hiyo Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema amefarijika sana na Muitikio wa wananchi wa eneo hilo kushiriki zoezi la upandaji miti. “Binafsi nimefarijika sana kuona muitikio wenu katika shughuli hii muhimu kwa ustawi wa nchi yetu na Maisha yetu”. Alisema Mhe. Makongoro.
Aidha, katika taarifa yake Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri Bi. Pellagia Shirima amesema Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ilianza kujengwa mwezi Machi, 2019 baada ya kupata fedha za ujenzi kutoka Serikali Kuu. Katika Kipindi cha mwaka 2018/2019 hadi 2022/2023 Halmashauri ilipokea fedha Shilingi Bilioni 2.76 kwaajili ya ujenzi wa majengo ya Hospitali ambapo shilingi Bilioni 2.69 ni kutoka serikali kuu na shilingi Milioni 70 ni fedha za Mapato ya ndani. Mapokezi ya fedha hizi yamewezesha kujengwa kwa majengo 12 ikiwemo nyumba ya mtumishi ya 3 in 1 na Hospitali ilishaanza kutoa huduma tangu tarehe 03 Aprili, 2023
RC Makongoro ametoa wito kwa uongozi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha miti yote iliyopandwa katika eneo la Hospitali inatunzwa vizuri na pia amesisitiza uhamasishaji wa upandaji miti katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri zote za Mkoa wa Manyara unaendelea ili kufikia lengo la upandaji miti 1,500,000 kwa mwaka kwa Mkoa mzima.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.