Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga ameongoza kikao cha Kwanza cha Bodi ya Barabara kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa leo Novemba 28, 2023 kikiwa na lengo la kujadili hali ya miundombinu katika Mkoa huo.
Katika kikao hicho, pamoja na mambo mengine agenda kubwa zilikuwa ni pamoja na kusoma na kuthibitisha muhtasari wa kikao kilichofanyika Novemba 28, 2022, kupokea taarifa ya utekelezaji wa mpango wa ujenzi na matengenezo ya Barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na zile zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Aidha, katika taarifa yake Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Manyara Injinia Dutu Masele amesema Wakala hiyo inasimamia mtandao wa Barabara wenye urefu wa km 1,657, kati ya hizo Km 207 ni Barabara kuu na Km 1,450 ni Barabara za Mkoa. Pia katika taarifa hiyo Injinia Masele amesema Kilomita 207 za Barabara Kuu zote ni za lami na Km 51 za Barabara za Mkoa ni za lami na kufanya jumla ya barabara za lami kuwa km 258.
Injinia ameeleza kuwa TANROADS Manyara imeidhinishiwa jumla ya Shilingi Milioni 2,946.110 kwa mwaka wa fedha 2023/24 kwa ajili ya kutekeleza kazi za maendeleo ikiwa ni pamoja na ukarabati kwa kiwango cha changarawe na ujenzi kwa kiwango cha lami na zege hasa hasa milimani. Mpaka kufikia tarehe 15 Novemba, 2023 jumla ya miradi minne (4) kati ya 7 imekwishapata Wakandarasi na wanasubiri kusaini mikataba kwa ajili ya kuanza kazi. Aidha, miradi mingine mitatu (3) ipo katika hatua za mwisho za manunuzi.
Mhe. Mkuu wa Mkoa akijibu swali la Mjumbe kuhusiana na uharibifu wa Barabara unaotokana na mifugo, amewaagiza Viongozi wote kuanzia ngazi ya Halmashauri kutoa ushirikiano katika kuwatia hatiani wote watakao jihusisha na uharibu huo wa Miundombinu. RC. Sendiga amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia usafi katika maeneo ya barabara na madaraja huku akitaka suala la upandishaji hadhi barabara kuanzia katika ngazi ya Halmashauri.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.