Kampuni ya Carbon Tanzania imekabidhi hundi ya Bilioni 4.7 kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo katika Ukumbi wa White Rose Babati Mkoani Manyara kwa Utunzaji wa Mazingira na baadae hundi hiyo kukabidhiwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga.
Mhe. Jafo ameipongeza Kampuni ya Carbon Tanzania kwa kufanya Biashara ya Hewa ya Ukaa kwani imesaidia katika suala zima la utunzaji wa mazingira na kutengeneza fursa kubwa ambayo imewawezesha kupata mapato nje ya vyanzo vingine. Waziri huyo amesema kuwa Wizara imekuja na miongozo na kanuni za biashara ya hewa ya ukaa katika Taifa letu.
Aidha, Mhe. Waziri ameongeza kuwa takribani makampuni 53 yameanza kufanya biashara ya hewa ya ukaa. Vilevile ameishukuru Kampuni hiyo kwa kuwa wawazi katika biashara hususani suala la mapato hiyo ni hatua nzuri katika ukuaji wa kibiashara kwa ujumla. Mhe. Jafo amewataka wananchi kutunza misitu kwani misitu ni mali na inapaswa kusimamiwa ili kupunguza/kuondoa uharibifu wa mazingira.
Mkurugenzi wa Carbon Tanzania Bw.Alphan Jackson amesema kuwa kutunza vyanzo vya maji, kulinda misitu ni jukumu la kila mmoja wetu kulinda na hii imesaidaia sana katika biashara ya hewa ya ukaa.Ameishukuru Serikali kwa kuweka mfumo rahisi katika shughuli za biashara ya hewa ya ukaa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga ameishukuru Kampuni ya Carbon Tanzania kwa hundi amabyo amepatiwa na kwa kazi nzuri ya utunzaji wa mazingira na Wananchi wamepata Elimu juu ya faida ya utunzaji wa misitu. Vilevile, Mhe. Sendiga ameongeza kuwa takribani wananchi 64,000/= wamenufaika na mradi huo wa utunzaji wa hewa ya ukaa ambapo baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Kiteto na Wilaya ya Mbulu wameanza kunufaika na mradi wa hewa ya ukaa tangu mwaka 2017.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.