Kikao cha wahandisi na wakuu wa Idara za Miundombinu kimefanyika leo 23/07/2024 katika Ukumbi Na. 76 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara. Akifungua kikao hicho cha kisekta, Katibu Tawala wa Manyara Bi. Mariam Muhaji amesema, anatambua umuhimu wa wahandisi na anafahamu changamoto wanazokabiliana nazo katika kazi zao. Aidha,Katibu Tawala ameendelea kusisitiza wahandisi wazingatie taaluma zao katika kufanya kazi zao. Vile Vile, amewaagiza wahandisi wote wa halmashauri kuimarisha usimamizi wa miradi ya ujenzi inayotekelezwa kwenye maeneo yao ikiwemo ile inayotekelezwa kwa fedha zinazopitia Sekretarieti ya Mkoa. Ameelekeza ushirikishwaji wa wahandisi wa halamashauri ufanywe na wahandisi wa Sekretarieti ya mkoa ili kupunguza gharama za usimamizi na kuongeza ubora wa kazi.
Katika hatua nyingine, Katibu Tawala wa Mkoa ametoa maelekezo kwa kila halmashauri kutoa kipaumbele katika ukamilishaji.wa miradi viporo ambapo inatakiwa ifikapo.mwezi Novemba 2024 viporo vyote viwe vimemalizika. Ameendelea kuwaasa wahandisi kujipanga vema kwa mwaka huu mpya wa fedha ikwemo.kuandaa mipango ya manunuzi na kuiwasilisha mapema kuepuka kuchelewa kuanza utekelezaji. Katibu Tawala wa Mkoa amesema, yeye mwenyewe atatembelea wilaya zote kwa zamu ili kujionea hali halisi ya utekelezaji wa Miradi.
Akiongea wakati wa kumkaribisha Katibu Tawala wa Mkoa, Bw. Dominick Mbwete ambaye ni Katibu Tawala wa Utawala na Rasilimali watu amesema, vikaokazi hivi vitakuwa ni endelevu na ametoa wito kwa washiriki kushiriki mjadala wa kina na kutoa mapendekezo ya utatuzi wa changamoto za miradi inayotekelezwa.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.