Mkoa wa Manyara umepokea zaidi ya Shilingi Bilioni 700 ndani ya kipindi cha miaka minne fedha ambazo zimeelekezwa kutumika kwenye miradi ya Maendeleo katika Sekta za Afya, Elimu, Maji, Utalii na Mali asili, umeme pamoja na miundombinu ya Barabara.
Pamoja na miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa ,inaelezwa kuwa ipo miradi ya kimkakati ambayo ni ujenzi wa soko la madini Mererani Wilaya ya Simanjiro na ujenzi wa Stendi ya Mabasi Katesh, Wilaya ya Hanang' ambapo Shilingi Bilioni10 zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa miradi hiyo ambayo itakamilika hivi karibuni.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga wakati akifungua kikao Cha 39 Cha kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Manyara tarehe 18 Februari 2025, mbele ya Wakuu wa Wilaya, Wabunge, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmshauri, Vyombo vya usalama na wadau mbalimbali wa Maendeleo.
"Katika Sekta ya Elimu Mkoa umepokea billion 112, fedha ambayo imetumika katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia. Vilevile, zaidi ya shilingi bilioni 27 zimetolewa kwenye Sekta ya Afya, fedha ambazo zimetumika katika kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo vituo vya kutolea huduma za afya na ununuzi wa dawa na vifaa tiba,
Shilingi Bilioni 29.3 zimetolewa katika Sekta ya Maji Vijijini, ambapo kupitia miradi mbalimbali iliyotekelezwa upatikanaji wa maji umeongezeka kutoka asilimia 56 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 71 mwaka 2025. Kwa upande wa Barabara za vijijini na mijini, kiasi cha shilingi Bilioni 49.2 kimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Barabara. Upatikanaji wa umeme umeendelea kuongezeka hususan vijijini, ambapo zaidi ya shilingi Bilioni 300 zimetumika katika kutekeleza miradi.
Amesema hivi Sasa Mkoa wa Manyara umekua na maendeleo makubwa ikilinganishwa na hapo awali huku akisema mbali na maendeleo yaliyopo katika Sekta ya Elimu,Afya na miundo mbinu ya Barabara lakini Sekta ya Utalii imekuwa kwa kasi ambapo watalii milioni 1 na laki 4 wamekuja kutalii katika hifadhi za Tarangire na Manyara kwa kipindi Cha miaka 4.
"Mazingira ya utalii yameendelea kuboreshwa ndani ya hifadhi za Tarangire na Manyara ambapo zaidi ya bilioni 7.8 zimeingia katika Mkoa wetu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba miundombinu mbalimbali katika hifadhi hizo inaboreshwa. Jitihada zinazoendelea kuchukuliwa ikiwemo uhamasishaji uliofanyika kupitia filamu ya “The Royal Tour”, jumla ya watalii milioni 1 na laki 4 wameingia ndani ya hifadhi hizo". Sendiga amesema
Wakati wa Kikao hicho, Sendiga alizungumzia suala la Kilimo kuwa Serikali imetoa Shilingi Bilioni 8.5 kwa ajili ya ujenzi wa Skimu ya umwagiliaji katika Wilaya ya Mbulu ikiwa na lengo la kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Manyara wanafanya Kilimo Cha umwagiliaji katika kipindi chote cha mwaka badala ya kutegemea mvua pekee. Ameongeza kuwa Kila mmoja anawajibu wa kutunza rasimali zaTaifa pamoja na miundombinu iliyowekwa.
Aidha, Kwa upande wake katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Mipango na Uratibu Lusungu Mwilongo, amesema Kwa mwaka wa fedha 2025/26 bajeti ya Mkoa wa Manyara ni shilingi bilioni 302.9 ambapo kati ya fedha hizo shilingi bilioni 78.7 ni Kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.