Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbert Sendiga, leo Februari 17, 2025 ameongoza kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Manyara kilichoshirikisha wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA, Wakala wa Barabara Tanzania TANROAD, wabunge wa Mkoa wa Manyara pamoja na Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri.
Akiongoza kikao hicho RC Sendiga, ametoa onyo kwa wafugaji wanaopitisha mifugo yao kwenye barabara kuacha tabia hiyo ili kuepusha uharibifu mkubwa wa barabara na kuwaagiza Halmashauri kutoa elimu kwa wafugaji kwenye maeneo yao kuhusu umuhimu wa kutunza barabara.
Aidha, RC Sendiga amewaelekeza Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA), kuwa mikataba ya miradi mbalimbali isisainiwe ikiwa fedha za kutekeleza miradi hiyo hazipo ili kuepuka lawama kutoka kwa wananchi badala yake pesa zinapopatikana ndipo mikataba hiyo isainiwe.
Sambamba na hilo RC Sendiga, ameelekeza wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA Mkoa wa Manyara kuchonga barabara katika eneo la Kilimani Wilayani Hanang na maeneo mengine ambapo Barabara ni korofi.
"TARURA kesho asubuhi nataka nione mnafanya kazi kule mlimani, kachongeni ile barabarani sababu kule kuna athari kubwa sana barabara ile haipitiki na wananchi wanapita katika barabara ya shule ya nangwa, geti halifungwi sasa ni hatari wa watoto wale wakike." Sendiga amesema
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho wameshauri kutungwa kwa sheria ndogo ya kupiga faini wafugaji wanaopitisha mifugo kwenye barabara na jukumu la kusimamia wakabidhiwe watendaji wa Kata na Vijiji ili iwe rahisi kubaini uharibifu mapema.
Katika mwaka wa fedha 2024/2025 TARURA Mkoa wa Manyara imetengewa Shilingi Bilioni 2,757.185 kwa ajili ya utengenezaji wa barabara kwa kiwango cha lami na changarawe.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.