Wajasiriamali Mkoani Manyara wanatarajiwa kugaiwa vitambulisho elfu arobaini na sita kwa kwa njia ya kieletroniki.
Akizungumza leo Alhamis na Makatibu Tawala, Maafisa Biashara na Wataalamu wa TEHAMA kutoka katika wilaya zote za Mkoa wa Manyara wakati wa ufunguzi wa mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkuu wa Mkoa ya jinsi ya kuwaandikisha wafanyabiashara hao Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Dkt. Damas Kayera aliwataka wataalamu hao kusilikiza kwa umakini ili wapate kurekodi taarifa za Vitambulisho kwa walengwa kwa uangalifu mkubwa kwenye mfumo maalum na kuwataka kila muhusika kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
“Maafisa biashara na Maafisa TEHAMA jukumu hili mmepewa na litakuwa sehemu ya majukumu yenu hivyo hakikisheni mnalitekeleza kwa uangalifu mkishirikiana na Maaafisa ngazi za kata na vijiji bila kuwasahau maafisa tarafa kwani wao ndio waliofanikisha kwa kiasi kikubwa katika zoezi la kwanza” Alisisitiza Kaimu Katibu Tawala.
Vitambulisho hivyo vitagawanywa kwenye Halmashauri kwa kuzingatia idadi ya wafanyabiashara na watoa huduma wadogo waliopo, wafanyabiashara wote wanatakiwa kujaza fomu za maombi na lazima fedha ziwekwe benki kwa kutumia control number 995040000014 na mgawo utafanyika kwa kila Halmashauri kwa mtiririko maalum wa namba na kwa mwaka huu vitambulisho vitaendelea kutolewa kwa bei ya shilingi elfu ishirini kama mwaka jana.
Wakizungumza baada ya mafunzo hayo Maafisa Biashara walitoa shukrani zao kwa Serikali kwa kufanya ugawaji wa vitambulisho kwa njia ya kieletroniki kwani utaondoa changamoto ya upotevu wa kumbukumbu kwani kila kitambulisho kitarekodiwa kwenye mfumo moja kwa moja.
Kwa upande wa Maafisa TEHEMA wa Halmashauri walisema kuwa ugawaji wa vitambulisho safari hii utakuwa na ufanisi mkubwa sana kwakuwa fedha zote zitakazokusanywa zitaingia Benki moja kwa na hivyo kuzuia wizi kwa baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu.
Mkoa wa Manyara awamu iliyopita ulipokea vitambulisho 60,000 na kufanikiwa kugawa vitambulisho 46,390 zoezi lililokuwa na changamoto kadhaa ikiwemo upotevu wa vitambulisho pamoja na kutokuweka kumbukumbu za wafanyabiashara wadogo waliopatiwa vitambulisho.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.