Maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kwa Mkoa wa Manyara yamepungua kutoka asilimia 1.4 hadi asilimia 0.46 kwa mwaka 2022 huku Wilaya za Kiteto na Simanjiro zikiongoza kwa kiwango cha juu cha maambukizi.
Wilaya ya Simanjiro na kiteto kila moja ina kiwango cha asilimia 1.2 cha maambukizi ambapo kwa mwaka jana pekee watu 3,872 waliugua malaria huku kati yao wanne wakithibitika kufariki baada ya kuugua malaria.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Charles Makongoro Nyerere, akizungumza leo Januari 20,2023 kwenye mkutano wa tathmini ya mkataba wa lishe kwa julai hadi Desemba 2022 na Uzinduzi wa zoezi la ugawaji wa vyandarua kwa wanafunzi wa shule za msingi wilaya za Kiteto na Simanjiro, amesema lengo la Mkoa ni kutokomeza ugonjwa huo kufikia mwaka 2030.
Amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kupambana na ugonjwa huo kwa kuongeza kasi ya upatikanaji wa vyandarua ngazi ya kaya kwa kugawa vyandarua vyenye ukubwa wa futi 5 kwa 6 kwa wanafunzi 44,884 wilaya ya Kiteto na wanafunzi 47,785 Simanjiro kwa shule zote za msingi za Umma na binafsi, zoezi ambalo litakuwa likifanyika kila mwaka
RC Makongoro aliwataka wakuu wa Wilaya, wakurugenzi wa Halmashauri na viongozi wa Dini wakatoe elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutumia vyandarua hivyo ili kujikinga na malaria.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.