Mkoa wa Manyara umegawanywa katika mikoa miwili ya ya kimadini ambayo ni Manyara na Simanjiro kutokana na upatikanaji mkubwa wa aina mbalimbali za madini yanayopatina kwa wingi Mkoani Manyara.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa madini Mh. Anjela Kairuki alipokuwa Wilayani Simanjiro katika ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu Hassan.
Waziri Kairuki alisema kwa kuwa Mkoa wa Manyara umebarikiwa aina mbalimbali za madini Wizara ya madini imeamua kutenga Mkoa mpya wa Kimadini ambao makao Makuu yake yatakuwa Mirerani ili kuongeza ufanisi wa kazi za madini katika Mkoa huo.
Akiwa katika siku ya pili ya ziara yake Mkoani Manyara Makamu wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan alitembelea na kukagua ukuta katika enero la Madini ya Tanzanite lililopo Mirerani na pia alitembelea kiwanda cha madini ya Kinywe (Graphite) pia kilichopo hukohuko Mirerani Wilayani Simanjiro na kuweka jiwela msingi la kiwanda hicho.
Akiongea na wamiliki pamoja na wafanyakazi wa kiwanda hicho Mhe.Makamu wa Rais aliwataka wamiliki wa kiwanda hicho kuongeza uzalishaji wa madini ya Kinywe kwani hicho ndo kiwanda pekee kinachozalisha madini ya Kinywe nchini Tanzania.
Madini ya Kinywe yanatumika kutengezea betri za magari,betri za simu pamoja na betri za saa,Vipuli vya mitambo pamoja na kutunza umeme kwa muda mrefu.
Akiongea kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais Mkuu wa Mkoa wa Manyara alisema kuwa Mkoa wa Manyara upo katika hatua za mwisho za kukamilisha idadi ya viwanda mia kwa kila mkoa katika kutimiza kauli mbiu ya “Mkoa wangu Kiwanda changu”
Mara baada ya kutembelea kiwanda cha Graphite Makamu wa Rais alifanya mkutano wa hadhara katika Mji wa Orkesumet kwa kuongea na wananchi wa wilaya ya Simanjiro.
Katika mkutano huo aliwataka wananchi kupambana na udumavu,maradhi ya ukimwi,ukeketaji na kuacha kuwaozesha watoto katika umri mdogo.
Kwa upande wa Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa Mh.Suleiman Jafo alisema kuwa Serikali tayari imeshatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Wilaya ya Simanjiro pamoja na Jengo la Halmashauri ya Wilaya kabla ya Juni 2019.
Ziara ya Makamu wa Rais inaendelea tarehe 16 Novemba wilayani Babati.
(Kwa picha mbalimbali na Video angalia sehemu ya Kituo cha Habari kisha nenda Maktaba ya Picha na Maktaba ya Video)
Imeandikwa Na: Haji A. Msovu
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.