Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga amezishukuru Taasisi zilizopo Mkoa wa Manyara, Kamati za maandalizi, Waratibu wa mbio za mwenge wa uhuru 2023, Waandishi wa Habari na wananchi wote wa mkoa wa Manyara kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha katika maadhimisho ya kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023. Akiongea na waandishi wa Habari ofisini kwake mapema leo, Mhe. Mkuu wa Mkoa pia, amevipongeza vyombo vya ulinzi na Usalama kwa kuweka mazingira ya Usalama kwa muda wote mkoani humo.
Maadhimisho ya kilele cha mbio za mwenge wa uhuru 2023 yaliambatana na ibada ya kitaifa ya kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika katika Kanisa la Parokia ya Roho Mtakatifu lililopo Mjini Babati na maadhimisho ya wiki ya vijana kitafa 2023 yaliyofanyika katika uwanja wa stendi ya zamani Babati Mjini.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maonesho ya kibiashara ambayo yanafanyika Mjini Babati kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 21 mwezi Oktoba 2023. Mhe. Sendiga amewataka wafanyabiashara kutumia maonesho hayo kutangaza biashara zao na kutangaza vivutio vya utalii pamoja na fursa za uwekezaji zilizpo Mkoani humo.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amelezea kuhusu Kampeni ya “Mama Samia nivishe viatu”, hii ni kampeni inayolenga kuwavisha viatu watoto wanaoishi mazingira magumu ambapo kwa sasa kampeni hiyo ipo mkoani Manyara na mpaka kufikia leo tarehe 17 Oktoba, 2023 kampeni hii imefanikiwa kuwavisha viatu watoto wasiopungua Elfu moja (1,000) kutoka katika shule Nne za wilaya ya Hanang’ na Wilaya ya Babati.
Mama Samia nivishe Viatu ni kampeni inayoongozwa na Msanii Steve Mengele maarufu kama Steve Nyerere, Msanii Yvonne Cherrie maarufu kama Monalisa, na wasanii wengine waliongozana nao. Kampeni hii kwa mkoa wa Manyara imelenga kuwavisha viatu watoto zaidi ya 2000 ambapo jumla ya pea 2800 za viatu zitatolewa ikiwa ni kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wanaotokea katika mazingira magumu wanapata viatu.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.