Na Nyeneu, P. R - Gallapo
Kufuatia maelekezo ya serikali kuwa maadhimisho ya sherehe za Muungano kwa mwaka huu zifanyike katika ngazi ya Mikoa nchini kote, Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Charles Makongoro Nyerere leo tarehe 26 Aprili, 2023 ameungana na wananchi wa Mkoa huo kuadhimisha kilele cha sherehe za miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika Katika Kijiji cha Gallapo Wilayani Babati ambapo kauli mbiu ni “Umoja na Mshikamano ndio Nguzo ya Kukuza Uchumi Wetu”.
Maadhimisho haya ambayo yameanza kufanyika kuanzia tarehe 17 Aprili, 2023 yaliambatana na shughuli mbalimbali za kijamii hususan upandaji miti, usafi wa mazingira na mashindano ya michezo na sanaa mbalimbali. Kadhalika, yaliambatana na Mashindano ya uandishi wa Insha kwa shule za Msingi na Sekondari na washindi washindi wa katika mashindano mbalimbali wamezawadiwa vyeti na fedha taslimu.
“Lengo kuu la Muungano huu ilikua ni kuendelea kudumisha uhusiano baina ya pande hizi mbili ambao umekuwepo kwa muda mrefu katika nyanja mbalimbali kama vile undugu wa damu, biashara, utamaduni, lugha na mahusiano ya karibu ya kisiasa baina ya vyama vya TANU na ASP ambavyo baadae viliunda Chama Cha Mapinduzi”. Alielezea Mhe. RC.
Vilevile Mhe. Makongoro amewapongeza sana wananchi wa Mkoa wa Manyara kwa kuuenzi Muungano kwa vitendo kwa kuimarisha Mshikamano, Ulinzi na Usalama unaowezesha watu wote kufanya kazi za uzalishaji mali kwa amani na utulivu na hivyo kukuza uchumi wa Mkoa na Nchi kwa ujumla.
Lakini pia amewapongeza kwa kushirikiana kwa pamoja katika kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo hadi sasa Mkoa umefanikiwa kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kama vile Kuongeza idadi ya Shule za Msingi na Sekondari ambapo hadi sasa Mkoa una jumla ya Shule za Msingi 642 na Sekondari 154, Kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za Afya mwaka hadi mwaka ambapo hadi sasa Mkoa una jumla ya Zahanati 186, Vituo vya Afya 29, na Hospital 12; Aidha, hali ya upatikanaji wa dawa muhimu imefikia 91%
Pia, Mhe. Mkuu wa Mkoa amemshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake mahiri ambapo ameendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Mkoa.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.