Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga, Katibu Tawala Mkoa wa Manyara pamoja na Mkurugenzi Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Novemba 20, 2023 wamehudhuria hafla ya utiaji saini katika mikataba 6 ya miradi ya maji yenye thamani ya Billioni 9 ambapo hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Babati Mkoani Manyara.
Mhe. Sendiga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya jitihada kubwa za kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji kwa kupeleka miradi ya maji kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara.
Aidha, RC Sending amesisitiza wakandarasi kukamilisha miradi hiyo kwa wakati na amewataka Wakuu wa Wilaya kusimamia miradi na kuangalia mikataba ili kumaliza miradi kwa wakati. Pia Mhe. Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa Mkoa wa Manyara una miradi mikubwa ya maji ipatayo 28 hivyo kufanya upatikanaji wa maji kufikia wastani wa asilimia 70.5.
Vilevile amesema kuwa miradi ya maji imeinua Sekta ya ufugaji katika Mkoa ikiwemo Ujenzi wa josho za kuoshea mifugo katika baadhi ya Wilaya za Mkoa huo. Kwa kipindi cha miaka 3 ya Uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan Mkoa umepokea jumla ya Bilioni 56 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji ambapo kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 Mkoa umepokea jumla ya Bilioni 21.7 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Sambamba na hilo, Mhe. Mkuu wa Mkoa amewataka wakandarasi kuajiri wazawa katika miradi hiyo ili kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi ikiwemo wajasiriamali wadogo kama mama lishe.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.