Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati Bwana Hamisi Malinga akiambatana na Maafisa Afya wa Halmashauri hiyo jana Machi 31,2020 wametekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe.Alexander Mnyeti alilolitoa siku ya Jumatatu Machi 30 alipotembelea Kiwanda cha kutengeneza vitakasa mikono kilichopo Babati Mjini na kuzitaka Mamlaka zote za Serikali za Mitaa zilizopo katika Mkoa wa Manyara kuhakikisha Vitakasa mikono vinasambazwa katika maeneo yote na hasa kwenye mikusanyiko ya watu.
Mkurugenzi Malinga na timu yake alitekeleza agizo hilo kwa kutembelea Mnada wa Dareda/ Ayalagaya na kutoa elimu juu ya kujinga na Ugonjwa wa Corona kwa wafanyabiashara na wateja katika maeneo ya Minada.
Mkurugenzi Malinga aliwaambia wafanyabiashara hao kuhakikisha wanachukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji yanayotiririka, kuacha kusalimiana kwa kushikana mikono, kuziba mdomo kwa maungio ya mkono wakati wa kupiga chafya na kutumia vitakatisha mikono ili kujikinga na ugonjwa huo kwani kinga ni bora kuliko tiba.
“Ndugu wafanya biashara na wateja wa eneo hili hakikisheni mnachukua hatua zote zinatotakiwa kuchukuliwa ili kujinga na janga hili la Corona” Alisema Mkurugenzi huyo.
Kuhusu Malalamiko ya vitakasa mikono kupanda bei Mkurugenzi huyo aliwahakikishia Wananchi kuwa Serikali ya Mkoa wa Manyara kwa kushirikiana na kiwanda cha kutengeneza vitakasa mikono cha Mati Super Brands kilichopo Babati Mjini itahakikisha bidhaa hizo zinapatikana kwa wingi na kwa bei nafuu katika maeneo yote ya minada na katika makazi ya watu pia.
“Kamati ya usalama ya Mkoa wa Manyara na Wilaya ya Babati tukiongozwa na Mkuu wetu wa Mkoa wa Manyara Mhe.Alexander Mnyeti ilitembelea kiwanda cha kutengeneza vitakatisha mikono kilichopo Babati na watuhakikishia bidhaa hizo zimezalishwa za kutosha na zitauzwa kwa bei ambayo kila mwananchi atamudu kuinunua” Aliongeza Mkurugenzi Malinga.
Akizungumza katika mnada huo Meneja masoko wa kiwanda hicho Bwana Mvungi alisema kuwa wametengeneza vitakasa mikono kwa kila ujazo na bei tofauti kulingana na kipato cha Mtanzania wa kawaida.Bei ya kiwandani ya bidhaa hizo ni kuanzia shilingi 1500 hadi 125000 kutegemeana na ujazo.
Kabla ya kumkaribisha Mkurugenzi Afisa Afya wa Halmashauri ya wilaya ya Babati Bwana Suten Mwabulango aliwaambia wafanyabiashara mnadani hapo watumie elimu watakayoipata kuwafikishia ujumbe wengine kwenye minada mbalimbali na hata Nyumbani kwao kwa familia zao kwani jukumu la kuelimisha ni la kila mmoja wetu.
“Nawashauri ndugu zangu hakikisheni mnaitumia elimu mtakayoipata hapa kuwafikishia na wengine kwenye minada mnapozunguka na hata majumbani kwenu” Alisisitiza Afisa Afya huyo.
Akiongea kwa niaba ya Wafanyabiashara wa Minada wote Mwenyekiti wa Minada Bwana Khalifa Ally aliwataka wafanyabiashara wenzake kufuata ushauri unaotolewa na wataalamu ili kujikinga na maradhi hayo na kuwahakikishia wataalamu hao kuwa wamejitahidi kuweka ndoo za kunawia mikono kila mahali pamoja na kuweka Jeshi la akiba ili kuwalazimisha wananchi kunawa mikono waingiapo na kutoka mnadani.
Elimu ya kujikinga na mlipuko wa Corona katika Mkoa wa Manyara inaendelea kutolewa kila sehemu ili kujikinga na ugonjwa huo.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.