Na, Ruth Kyelula, Manyara RS
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amewataka wamiliki wa migodi ya Tanzanite, Mirerani Wilayani Simanjiro, wajikite katika kupunguza ongezeko la ugonjwa wa TB na Silicosis kwa wachimbaji wao kutokana na vumbi la madini kuathiri mapafu ya wachimbaji, wawapo katika zoezi la uchimbaji madini kama ivyoainishwa kwenye utafiti uliofwanywa na mtafiti kutoka chuo kikuu Ardhi, Dar-es-Salaam (Dr. Manti M. Nota) kwa kushirikiana na Gem Legacy.


Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe.Queen Sendiga, akizungumza na Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Bi. Maryam Muhaji, katika kikao cha wamiliki wa migodi ya Tanzanite, Simanjiro.
Aliyasema hayo wakati wa kikao chake na wamiliki wa migodi ya Tanzanite pamoja na wataalamu mbalimbali wa ngazi ya Mkoa na Wilaya, kilichofanyika katika ukumbi wa Mazubu Grand Hotel, katika mji mdogo wa Mirerani,Wilayani Simanjiro, Oktoba 20, 2025.




Baadhi ya wamiliki wa migodi ya Tanzanite, Wilayani Simanjiro, wakifuatilia kikao cha mhe. RC.
"Niwaombe wamiliki wa migodi muweze kuchimba visima vya maji ama muweke ma tanki kwenye migodi yenu, ili mkiwa kwenye shughuli zenu za uchimbaji mmwagie maji kama wataalamu walivyoshauri kwenye utafiti ili kupunguza vumbi jingi linaloingia kwenye mapafu na kupelekea TB na Silicosis kwa wachimbaji badala yake tuchimbe na maji ili kulinda afya zetu na wafanyakazi wetu." Alisema Sendiga.



Aidha amewataka wamiliki wa migodi hiyo, kuhakikisha usalama wa afya za wachimbaji wao wa madini, pamoja na kuwapa elimu namna ya kujikinga dhidi ya magonjwa hayo lakini pia wawe na utaratibu wa ucheki afya zao mara kwa mara ili pia waweze kupata matibabu mapema.


Kwa upande mwingine Mhe.Sendiga amewaasa wamiliki hao wa migodi kufanya (CSR) kurudisha sehemu ya wanachopa kwa jamii,ili jamii nayo inufaike na uwepo wa migodi hiyo katika maeneo wanayoishi. Na aliwashukuru kwa mwaka jana kuweza kutoa CSR ya milioni arobaini (40) kwa jamii.



Mwisho Mhe. Sendiga aliwakumbusha na kutoa wito kwa wamiliki hao wa migodi ya Tanzanite, kushiriki uchaguzi mkuu, ifikapo Oktoba 29, 2025, watumie haki yao ya kikatiba waende kwenye vituo vya kupigia kura na wapige kura kwa Amani na utulivu.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.