Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe.Joseph Joseph Mkirikiti amewataka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi hasa wanaoishi mbali na mijini juu ya Huduma ya Usajili wa Vizazi na Vifo kwa njia ya Kielektroniki (E-HUDUMA) ili huduma hiyo iwafikie wananchi wengi iwezekanavyo na kuondoa usumbufu kwa kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
Mheshimiwa Mkirikiti ameyasema hayo leo Agusti 24, 2020 alipokuwa akizindua mafunzo ya huduma ya usajili wa vizazi na vifo kwa njia ya Kielektroniki kwa Wakurugenzi wa Halmashauri,Maafisa Taarafa,Maafisa Elimu wa Halmashauri na Maafisa Elimu kata katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Babati Mkoani Manyara.
“ Nitumie nafasi hii kuwataka RITA mfike maeneo yote kutoa elimu juu ya kutumia huduma hii ili tuweze kuwapunguzia wananchi usumbufu na gharama kwa kusafiri umbali mrefu kufuata vyeti katika Ofisi za RITA ambazo mara nyingi zinakuwa katika Ofisi za Wakuu wa Wilaya”Alisema Mhe.Mkirikiti.
Huduma hizo za usajili wa vizazi na Vifo kwa njia ya Kielektroniki zinamwezesha Mwananchi kutumia simu za kisasa popote alipo kufanya maombi ya vyeti vya kuzaliwa,kuhakiki cheti cha kuzaliwa au kifo, kutuma,kutuma maombi mapya ya vyeti vya kuzaliwa au vifo na kuhakiki cheti cha kuzaliwa au kifo kwa urahisi.
Ili kupata huduma hiyo tembelea tovuti ya RITA www.rita.go.tz kisha bonyeza kitufe kilichoandikwa “E- HUDUMA”, Fungua akaunti ya usajili itakayokuwezesha kutuma na kufuatilia mrejesho wa maombi yako halafu Chagua huduma unayoihitaji na fuata muongozo/maelekezo yaliyotolewa.
Mfumo huu utatoa fursa kwa wananchi wengi kupata cheti cha kuzaliwa akiwa nje ya eneo (Wilaya) alipozaliwa au tukio la kifo lilipotokea.
Wakati huohuo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara amefanya Kikao na Wafanyabiashara wa Mkoa huo na kuwataka kutafuta fursa zilizomo Mkoani Manyara ili kuwekeza na kuleta maendeleo kwa wananchi wa Mkoa hu.
Aliyasema hayo leo alipokuwa akiongea na makundi mbalimbali ya wafaanyabiashara wa Mkoa wa Manyara baada ya kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara Mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa amewataka Wafanyabiashara hao kujenga mahusiano mazuri na Serikali yao na kuhakikisha wanazitambua fursa zilizopo na kuzifanyia kazi.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.