Mkuuwa Mkoa wa Manyara Mh.Alexander Mnyeti ameitaka Halmashauri ya Mji wa Babati kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza mapato ya Halmashauri hiyo.
Mh.Mnyeti amesema hayo jana Jumamosi alipokuwa akihutubia Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo lililokaa kujadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Mheshimiwa Mnyeti alisema kuwa haridhishwi na kiwango cha ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri hiyo ambayo kwa mwaka inakusanya shilingi Bilioni 1.2 tu.
“Kwa mapato haya ya Bil. 1.2 hakuna mnachokifanya,hamuwezi kuendesha Halmashauri kwa mapato madogo kiasi hiki” Alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Akitolea mfano kwa Halmashauri zinazomiliki timu za mpira kama Ruangwa,Mbeya na Kinondoni Mh.Mnyeti aliwataka Madiwani na Wataalam wa Halmashauri hiyo wakajifunze juu ya kuendesha timu na viwanja vya michezo kama uwanja wa Kwaraa uliopo ndani ya Halmshauri ya Mji wa Babati kwa kuujengea majukwaa ili viingilio vitokanavyo na uwanja viingie katika mapato ya Halmashauri.
Mheshimiwa Mnyeti alitoa ahadi ya kutafuta wafadhili wa kutengeneza sehemu ya kuchezea na kuwataka Madiwani kuanza mchakato wa ujenzi wa uzio uwanjani hapo.
“Zungushieni uzio uwanja wote mimi pale pa kuchezea nitawatafutia mdhamini atawajengea” Alisema Mheshimiwa Mnyeti.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara yupo kwenye ziara ya kutembelea mabaraza ya Madiwani Mkoani Manyara yanayojadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali.
(Kwa picha mbalimbali angalia sehemu ya Kituo cha Habari kisha nenda Maktaba ya Picha)
Imeandikwa na:Haji A.Msovu
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.