Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe.Alexander Mnyeti amewataka wakazi wa mkoa huo kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Serikali na wataalamu wa Afya ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona unaoambukiza na kuua kwa kasi Duniani.
Aidha amewaonya wafanyabiashara wanaouza vitakasa mikono (Sanitizer) wenye tabia ya kubadilisha bidhaa husika na kupoteza ubora uliopo na wanaouza kwa bei ya juu tofauti na maelekezo ya Serikali na kwamba watakaobainika kufanya hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Mhe.Mnyeti amezungumza hayo siku ya Jumatatu Machi 30 alipotembelea kiwanda cha Mati Super Brands Ltd cha mjini Babati ambacho kimeamua kushirikiana na Serikali kutengeneza vitakasa mikono ili kupambana na virusi vya Corona na kuviuza kwa bei elekezi ya serikali.
“Tujitahidi sana kujikinga, hicho ndo sisi tunaweza kwani tukisubiri ugonjwa uingie,usambae halafu ndo tutafute matibabu itatusumbua sana, kwa hiyo tujitahidi sana kwenye kujikinga kabla ugonjwa haujasambaa” Alisisitiza Mnyeti.
Katika ziara yake kiwandani hapo Mkuu wa Mkoa ameupongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kujali afya za wananchi huku akiwataka waendelee kuzalisha kwa wingi bidhaa hizo ili wananchi wa Mkoa wa Manyara na Mikoa ya jirani waweze kuzipata kwa urahisi. Pia ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kuhakikisha bidhaa hiyo inazalishwa kwa wingi na kusambazwa katika maeneo yote ndani na nje ya Mkoa yenye uhitaji.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Bwana Missaile Musa ameeleza kuwa bidhaa hiyo itasaidia sana katika maeneo yenye shida ya maji, hivyo atawasiliana na wilaya za pembezoni ili waisambaze kwa wananchi kwa kuwa uhitaji ni mkubwa sana.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mati Super Brand Ltd Bwana David Mulokozi amesema wameamua kutengeneza Vitakamkasa mikono ili kuwasaidia wananchi waweze kujikinga na virus vya covid 19 kwa kuwauzia kwa bei ambayo mwananchi wa kawaida anaweza kumudu kununua kwani wanauza kuanzia Shilingi 1500 Mil 50, shilingi 2500 Mil 100, Lita tatu ni Shilingi 75000 na Lita tano ni shilingi 125000.
Kiwanda cha Mati Super Brand Ltd kinachojihusisha na utengezaji wa Vinywaji vikali kimeanza kutengeneza vitakasa mikono mara baada ya kufumuka kwa ugonjwa wa Corona na nchi kuingia kwenye uhitaji mkubwa wa Vitakasa mikono
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.