Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe.Alexander Mnyeti amezipongeza Halmashauri zote saba za Mkoa wa Manyara kwa kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo kwa miaka ya fedha ya 2016/17,2017/18 na 2018/19 kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali.
Mheshimiwa Mnyeti alitoa pongezi hizo akiwa katika ziara ya kutembelea Mabaraza ya Madiwani ya kupitia hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali yaliyofanyika katika makao Makuu ya Halmashauri hizo kuanzia tarehe 28 hadi 29 mwezi Mei.
“Kwa kweli lazima niwapongeze Madiwani na Wataalam wote katika kila Halmashauri ya Mkoa wa Manyara kwa kuhakikisha tunapata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo kwani miaka ya nyuma hali haikuwa kama ilivyo sasa,hongereni sana”Alisema Mkuu wa Mkoa.
Pamoja na pongezi hizo pia alimtaka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali kuhakikisha baadhi ya hoja kama za upungufu wa watumishi na kupewa ukuu wa Idara/kitengo zinaondolewa kwa Halmashauri kwa kuwa hizo ni hoja za kisera na kamwe hazihusiani na Madiwani kwani Madiwani hawana uwezo wa kutatua tatizo la upungufu katika Halmashauri.
“Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali kuna baadhi ya hoja kwa kweli ni vema mkawakague Wizara ya Utumishi na TAMISEMI ndo muwaulize kwanini hawaleti watumishi na kuwapandisha vyeo watumishi waliokaimu Idara/Vitengo kwa muda mrefu Mkoa wa Manyara” Alisisitiza Mheshimiwa Mnyeti.
Akijibu hoja hiyo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali Mkoa wa Manyara Bwana Paschal Mawago alisema kuwa watajitahidi kukaa na wataalam wa Halmashauri kuhakikisha kuwa hoja zote za kisera zinafutwa na pia aliwataka wataalam kufika katika Ofisi za Mkaguzi zilizopo Babati wakati wowote wapatapo vielelezo vya baadhi ya hoja ili kuzifuta na kuzifunga.
Akiwa katika Baraza la Madiwani Wilayani Kiteto Mkuu wa Mkoa pia alishuhudia Diwani wa viti Maalum Mheshimiwa Zamda kutoka CHADEMA alitumia nafasi hiyo kukihama chama chake na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Mheshimiwa Mwenyekiti kuanzia leo tarehe 28 Mei mimi nikiwa kama Diwani wa CHADEMA nimeamua kujiunga na CCM bila kushawishiwa na mtu yoyote kwani sioni jambo la maana watakalofanya CHADEMA ambalo Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli hajafanya.Alisema Mheshimiwa Zamda.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa pia alitumia ziara hiyo kuwaaga na kuwatakia kila la heri Madiwani na Wabunge wote wa Mkoa wa Manyara kwani Mabaraza yote ya Madiwani yanatarajiwa kuvunjwa kuanzia tarehe 10 Juni 2020 ili kupisha mchakato uchaguzi Mkuu wa Madiwani,Wabunge na Rais kuanza na pia kuwataka Wakuu wa Idara kusimamia vizuri Halmashauri katika kipindi hicho ambacho Halmashauri hazitakuwa na Mabaraza ya Madiwani.
“Kwa kuwa hili ni Baraza la mwisho kabla ya Baraza kuvunjwa nitumie nafasi hii kuwatakia kila la heri Mdiwani katika uchaguzi ujao wa mwezi Oktoba, naamini asilimia zaidi ya tisini mtarudi baada ya uchaguzi na pia katika kipindi hiki nawataka Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kuhakikisha mnadhibibiti matumizi ya fedha” Alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
(Kwa picha mbalimbali angalia sehemu ya Kituo cha Habari kisha nenda Maktaba ya Picha)
Imeandikwa na:Haji A.Msovu
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.