Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Joseph Mkirikiti amewataka wamiliki wa vitalu vya uwindaji mkoani humo kuacha kufanya shughuli za kilimo kwani kufanya hivyo kunaleta uharibifu wa mazingira na kuwafanya Wanyama wakimbie kwa kuhofia usalama wao.
Mhe.Mkirikiti ameyasema hayo jana wakati alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa vitalu vya uwindaji katika wilaya ya Simanjiro kujionea jinsi wawindaji hao wanavyotumia fursa hiyo kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na serikali na kukuta baadhi ya wawindaji wameanzisha shughuli za kilimo katika vitalu hivyo.
“Mimi na kamati ya usalama hatujaridhirishwa na mmiliki wa vitalu hivi kwa sababu tunataka kujua maslahi ya Serikali na maslahi ya wananchi katika eneo hilo kwani tumeona maeneo mengi yaliyotengwa kwa shughuli za uwindaji yanatumika kwa shughuli za kilimo hivyo nawataka wamiliki waote wa vitalu vya uwindaji kuacha mara moja kufanya sghuli za kilimo katika maeneo haya” Alisema Mhe. Mkuu wa Mkoa.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amesema kuwa Pamoja na wawindaji hao kuwa na vitalu lakini bado wananunua maeneo ya vijiji bila kufuata taratibu na kuwataka wawindaji kufuata taratibu za kununua maeneo hayo.
“Kila mtu aliyenunua maeneo ya Vitalu vya uwindaji lazima afuate taratibu za ununuzi na pia nawataka wote walionunua maeneo wakaripoto kwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro ili Serikali ijue kuwa umiliki huo una uhalali gani kwani kwa taarifa tulizonazo wananchi wa maeneo haya wanauza maeneo kwa bei rahisi bila ya kufuata taratibu za uuzaji wa maeneo” Alisema Mhe.Mkirikiti.
Mkoa wa Manyara una vitalu 16 vya uwindaji ambapo Mkuu wa Mkoa huo aliwataka wawindaji wote katika mkoa kuhakikisha wanatambulika kisheria katika ofisi za wakuu wa wilaya kwani Mkuu wa Wilaya ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama katika eneo husika.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.