Naibu waziri Ofis ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh.Mwita Waitara amewataka watumishi wa umma Mkoani Manyara kuacha urasimu na kufanya kazi kwa bidii ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Mheshimiwa Mwita ameyasema hayo siku ya Alhamis katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati alipokuwa na kikao na watumishi kutoka Halmashauri za Wilaya na Mji wa Babati alipofanya ziara ya siku tatu Mkoani Manyara.
“Ndugu zangu watumishi wa umma jitahidini kufanya kazi zenu kwa bidii ili kuwaletea wananchi wetu maendeleo kwani tukishindwa kuwaletea maendeleo wananchi tutawafanya wananchi kuichukia seriukali yao” Alisema Mheshimiwa Naibu Waziri.
Katika kikao hicho Mheshimiwa Naibu waziri Mwita aliwataka watumishi wa umma kuteketeleza ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 kwa juhudi zote kwani ilani hiyo imeahidi maendeleo kwa wananchi wote.
Akizungumzia maslahi ya wafanyakazi Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI amewataka Wakurugenzi wote kushughulikia maslahi ya wafanyakazi wao ili kuondoa manung’uniko kwani wafanyakazi wakiwa na manung’uniko hata ufanisi kazini unapungua.
Akitolea mfano kwa watumishi saba wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati waliokaimu nafasi za ukuu wa Idara na Vitengo zaidi ya miezi sita Mheshimkiwa Naibu Waziri alisema “Hairuhusiwi mtumishi mwenye sifa za kuwa mkuu wa idara au kitengo kukaimu kwa zaidi ya miezi sita bila kupandisha cheo!!! Kama mtumishi ana sifa kwa nini mnachelewa kumpandisha cheo? Nataka maelezo juu ya hawa watumishi saba waliokaimu kwa kipindi kirefu bila kuthibitishwa” Naibu waziri alisisitiza.
Baada ya kikao hicho Mheshimiwa Naibu Waziri alitembelea miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya Afya,maji na Elimu iliyomo Halmashauri ya Mji wa Babati na Halmashauri ya Wilaya ya Babati.
Mheshimiwa Mwita Waitara ataendelea na ziara yake kesho kwa kutembelea Halmashauri ya Hanang’ na Keshokutwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto.
(Kwa picha mbalimbali na Video angalia sehemu ya Kituo cha Habari kisha nenda Maktaba ya Picha na Maktaba ya Video)
Imeandikwa Na: Haji A. Msovu
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.