Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI) Mhe. Festo Dugange, anayeshughulikia Afya amewataka wataalam wa Afya katika ngazi za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kujitafakari na kubadilika ili kuendana na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Aidha kwa yeyote atakayeshindwa kufanya hivyo ni vema akawa tayari kupisha watu wenye uwezo.
Akizungumza kwenye kikao maalumu cha kujitambulisha mbele ya Watumishi wa Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ndani ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Dugange, alisema, kutokana na mikakati iliyopo na mipango ya kusukuma sekta ya afya, nilazima kila mmoja ajitathimini kwa nafasi yake na majukumu aliyo nayo kama kweli anaitendea haki nafasi aliyo kabidhiwa.
Akiainisha vipaumbele muhimu Dkt. Dugange alisema, kubwa watakalo anza nalo ni uboresha wa upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi; uboreshaji wa mapato ametaja kama kipaumbele namba mbili huku akihimiza matumizi ya Mfumo wa GoTHOMIS, alisema suala la ukarabati mdogo mdogo kwenye vituo pamoja na maslahi na marupurupu ya watumishi yatategemea sana suala la uboreshaji wa mapato katika vyanzo vyote muhimu na hasa wakizingatia matumizi ya Mfumo.
“Katika ajenda hii ya mapato waganga wakuu wa Halmashauri wahakikishe baada ya tathmini ya ufatiliaji, yaonekane mabadiliko kwa macho ikiwepo vituo kupunguza utegemezi, ili kuweza kujifanyia baadhi ya mambo wao wenyewe”, alisema Dkt. Dugange na kuongeza kuwa, mbali ya boreshaji wa mapato vilevile ni lazima uboreshaji wa miundombinu iwe ni suala endelevu.
“Ni lazima pia tuboreshe miundombinu yetu na kuhakikisha ile asilimia ishirini ya ongezeko inayotajwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020 hadi 2025, tunaifanyia kazi mapema kuanzia sasa kwa bajeti tulizo zipanga lakini pia kwakuwatumia wadau wetu wa maendeleo tunaoshirikiana nao, bila kusahau uhamasishaji wa jamii kuanza shughuli za ujenzi kama mpango wa jamii unavyo elekeza”. Alisema Naibu Waziri huyo.
Awali kabla ya kuzungumza na watumishi hao, Mkurugenzi wa Tiba na Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Ntuli Kapologwe, alimpongeza na kisha kutoa taarifa fupi ya utendaji kazi mbele ya Naibu Waziri huyo, ambapo pamoja na mambo mengine, Dkt. Ntuli alimuelezea Naibu Waziri juu ya ujenzi wa miundombinu ya afya katika ngazi mbali mbali.
“Sisi katika suala zima la miundombinu, ndani ya miaka mitano tumefanikiwa kujenga vituo 487 na kati ya hivyo 293 tayari vimeanza kutoa huduma na vingine vikiwa katika hatua mbalimbali, vile vile tumefanikiwa kusimamia ujenzi wa Hospitali za Halmashauri 102, ambapo 99 ni zile zilizojengwa kwa fedha za Serikali na Wadau na Halmashauri mbili za Nyamagana na Arusha hawa walijizatiti na wameweza kujenga wao wenyewe kwa mapato yao ya ndani, aidha jumla ya Zahanati 1,198 zimekamilika, lakini pia kuna baadhi ya Mikoa inayofanya jitihada binafsi ikiwepo Mkoa wa Geita ambao wapo katika mpango wa kujenga Zahanati 100.” Alisisitiza Dkt. Ntuli
Mbali na ujenzi huo pia Dkt. Ntuli alielezea suala la maboma ya Zahanati, yapatayo 555 katika mwaka wa fedha wa 2020/21, ambapo katika hali ya sasa lazima kila Halmashauri, iweze kufanya maombi ya fedha zenyewe, utaratibu huo ambao ni mpya una lengo la kuonesha hatua na juhudi binafasi kwa kila Halmashauri. Aidha taarifa hiyo imeonesha mbali ya Zahanati vipo pia vituo vya Afya 52 ambavyo vilipata Milioni. 200 kila kimoja na sasa kila Kituo kitalazimika kuongezewa Milioni. 300 kila kimoja ili waweza kufikisha jumla ya Milioni. 500 ili wakamilishe ujenzi na kuanza kutoa huduma.
Katika Hatua Nyingine Dkt. Ntuli, alimfafanulia, Naibu Waziri juu ya tafiti tunduizi na kubaini baadhi ya Hospitali za Wilaya kama Sengerema na Kahama, ambazo zimekuwa zikipokea kina mama kwa ajili ya kujifungua wapatao 900 kila mwezi, hivyo ipo haja Hospitali hizo kuzipatiwa huduma za kibingwa kwani umbali wa Hospitali hizo na Makao Makuu zilipo Hospitali za Rufaa za Mikoa ni mbali.
“Mfano kwa Wilaya ya Kahama hadi Shinyanga Mjini ni zaidi ya Kilomita.102, hali inayochangia Vifo vya kina Mama kutokana na kusafirishwa umbali mrefu, kwa mantiki hiyo, tumeamua suala hili kuwapelekea wenzetu wa Wizara ya Afya, ili Hospitali hizi sasa ziweze kupewa hadhi ya Rufaa ya Mkoa na kupelekewa huduma za kibingwa”. Alisema Ntuli.
Dkt. Festo John Dugange, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri anayeshughulikia Afya Ofisi ya Rais-TAMISEMI tarehe 05 Desemba, 2020 na kuapishwa tarehe 09 Desemba, 2020 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Ikulu ya Chamwino Dodoma.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.