Katibu Tawala Mkoa wa Manyara Bwana Missaile Musa ameitaka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Rural Water Supply and Sanitation Agency –RUWASA) Mkoa wa Manyara kuhakikisha huduma za maji zinafika katika maeneo mengi Mkoani Manyara ikiwemo katika maeneo ya Shule,Zahanati na Vituo vya afya kwani sehemu hizo ni muhimu kuwa na huduma ya maji muda wote.
Katibu Tawala ameyasema hayo leo Jumatano wakati wa kikao cha Kamati ya Lishe Mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa jingo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara mara baada ya Kaimu Meneja wa RUWASA mkoa Mhandisi Wolta Kirita aliposoma taarifa ya hali ya upatikanaji wa maji Mkoani Manyara. Kaimu Meneja huyo alisema hali ya upatikanaji wa maji ni kwani mpaka sasa upatikanaji wa maji Vijijini ni asilimia 55, miji midogo upatikanaji ni asilimia 65 na pia Mamlaka ya Maji Babati BAWASA imeongeza eneo la kutoa huduma ya maji katika miji ya Galapo,Dareda,Bashneti na Mbulu hivyo kufanya sehemu kubwa ya Mkoa wa Manyara kuwa na vyanzo vya uhakika vya maji.
Akizungumzia changamoto za usalama wa maji yanayopatikana Mtaa wa Mrara na Bonga Kaimu Meneja wa RUWASA alisema kwa sasa wameshaanza kuchukua hatua za kufunga chujio kwa ajili ya kuchuja maji pamoja na kuweka mlinzi ili kusitokee uharibifu wa vyanzo vya maji.
“Tumeanza kuweka chujio la kuchuja maji katika chanzo cha maji Bonga,tukimaliza Bonga tutaweka Mrara ili kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama” Aliseme Mhandisi Kirita.
Akizungumzia juu ya Miradi ya Maji Mkoani Manyara Kaimu huyo wa RUWASA alisema RUWASA itahakikisha Wilaya zote za Mkoa wa Manyara zinapata maji ya uhakika na kwa kwa sasa kuna miradi ya Olchoronyori,Olbili Wilayani Simanjiro,Malangi katika Wilaya ya Babati na mradi mkubwa wa maji unatarijiwa kujengwa katika wilaya ya Kiteto utakaohudumia wilaya ya Kiteto na Wilaya ya Kongwa Mkoa wa Dodoma.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Manyara Bwana Missaile Musa alisifu kazi zinazofanywa na RUWASA Mkoa kwa kuhakikisha huduma za maji zinapatikana kwa uhakika.
“Kwa kweli pamoja na ugeni wako Mhandisi wa Maji lakini umejitahidi kuhakikisha umetembelea maeneo yote yenye changamoto za maji na kuzitatu” Alisema Katibu Tawala.
Akisoma Taarifa ya Lishe Moa Afisa lishe Mkoa wa Manyara Bwana Mabula Migata alisema ugawaji wa chakula kwa shule za Sekondari ni asilimia mia moja kwani shule zote 151 za serikali zilizopo mkoani Manyara zinagawa chakula kwa wanafunzi na kwa upande wa shule za msingi ugawaji wa chakula ni asilimia 80 ya shule zote za serikali zinazogawa chakula kati ya shule 603 za msingi zilizopo mkoani Manyara.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.