Na Nyeneu, P. R - Mjini Babati
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mh. Queen Sendiga amepokea Viatu pea 2,800 kutoka katika Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao ikiwa ni kampeni ya 'Mama Samia Nivishe Viatu'. Akizungumza katika makabidhiano hayo Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Ndg. Steve Mengele maarufu kwa jina la Steve Nyerere, amesema kampeni ya 'Samia Nivishe Viatu' lengo lake ni kuwapa tabasamu watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
"Kampeni ya Mama Samia Nivishe Viatu inasambaa Tanzania nzima, na sasa imefika Mkoa wa Manyara. Niwashukuru sana Viongozi wote wa Mkoa na Wilaya mpaka Vijiji kwa ushirikiano wao wanaounyesha kwetu hakika tumefarijika sana," amesema Steve Mengele.
Akitoa shukrani zake, Mhe. Queen Sendiga amesema kuwa jambo lililofanywa na taasisi hiyo imeacha alama katika mkoa wa Manyara hakika watabaki katika mioyo yao.
"Binafsi sina cha kusema zaidi ya AHSANTE hili mlilolifanya ni kubwa mno, hivi viatu vitasambaa shule zote za msingi zenye mahitaji maalum, niziombe pia taasisi nyingine kujitoa kuunga mkono maendeleo ya mkoa wetu," amesema Mhe. Sendiga.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati Bi. Anna Mbogo amesema ujio wa taasisi hiyo umeleta neema na faraja kwa jamii ya wana Babati.
Kampeni ya 'Samia Nivishe Viatu' imelenga kuwavika viatu jumla ya watoto 2,000 licha ya mkoa huo kupatiwa pea 2,800 na mpaka sasa jumla ya shule nne zimevalishwa viatu pea Zaidi ya 1,000.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.