Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga amewaagiza Makatibu Tawala Mikoa Tanzania Bara kusimamia vyema miradi yote ya maendeleo katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili ikamilike kwa wakati na kwa thamnai ya fedha iliyopangwa.
Mhandisi Nyamhanga ametoa kauli hiyo wakati akiongea na Uongozi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Manyara na Halmashauri za Babati Mji na Wilaya na wakati akikagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri hizo.
“Timu zote za Sekretarieti za Mikoa zinazosimamia miradi ya afya na miradi mingine zihakikishe kuwa kazi za miradi zinakamika kwa wakati uliyopangwa na kwa thamani ya fedha ile ile lakini pia utoaji wa huduma bora kwa wananchi ili kuleta tija”
Amesema miradi hiyo ni pamoja na ile ya sekta ya afya ambapo kuna ujenzi wa hospitali za Wilaya 67 unaotakiwa kukamilka mapema mwezi Juni, 2019, vituo vya afya 352 ambavyo ujenzi wake umebakia kwa baadhi ya vituo vya awamu ya tatu, miradi ya vikundi vya vijana, akina mama na watu wenye ulemavu kwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri husika, miradi ya barabara, stendi, elimu na mingine mingi inayotekelezwa katika Halmashauri zote nchini.
Aidha, Nyamhanga amesema katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali itajenga hospitali mpya za wilaya 27 na vituo vipya vya afya zaidi ya 52 ili kuboresha sekta ya afya nchini kama ilivyokusudiwa na Serikali ya Awamu ya Tano kuboresha afya za wananchi.
Katika hatua nyingine Nyamhanaga amesema kuwa Serikali inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kugharimia Elimu Bila Malipo amabapo jumla ya shilingi Bilioni 29.5 zinatolewa kila mwezi katika vituo vya kutolea huduma moja kwa moja.
Amewaasa watumishi wa Serikali katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuacha kufanya kazi kwa mazoea bali wajitume ili kutoa huduma bora kwa wananchi ambao ndio walengwa wakuu katika sekta zote.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Bw. Masaile Mussa akitoa taarifa ya Mkoa wa Manyara, amesema kuwa katika sekta ya elimu kiwango cha ufaulu kimeongezeka ambapo mwaka 2018 darasa la saba ni asilimia 70 na kidato cha nne ni asilimia 84 na ufaulu huo unaongezeka kila mwaka na lengo lao ni kupita asilimia 80.
Aidha, Mkoa wa Manyara umefanikiwa kutoa vitambulisho 60,000 vya Mhe. Rais walivyopatiwa Mkoa wa Manyara ambapo mpaka sasa wafanya biashara wadogo wapatao 38,726 wamepatiwa vitambulisho na bado wanaendelea kugawa ili kufikia malengo waliyojiwekea kwa kugawa vitambulisho vyote.
Mhandisi Nyamhanga anafanya ziara yake ya kikazi mkoani Manyara ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu ateuliwe kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI).
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.