Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Josephat Senkamba Kandege amesema Serikali imejiwekea mikakati wa kuhakikisha vituo vyote vya afya vilivyojengwa nchini vinakuwa na wataalam, vifaa vya kutosha kikiwemo kipimo cha Ultra-Sound ili kutoa huduma bora za afya kwa wananchi
Akijibu swali Bungeni leo lililotaka ufafanuzi juu ya mkakati wa Serikali wa kununua kipimo cha Ultra Sound katika Kituo cha afya cha Ujiji Mkoani Kigoma Mhe. Kandege amesema katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imeidhinishiwa zaidi ya shilingi milioni 15 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Ujiji kupitia mradi wa malipo kwa ufanisi kwa ajili ya ukarabati wa chumba kinachotumika kwa huduma ya mionzi na shilingi milini 45 kwa ajili ya ununuzi wa Ulta Sound
Anafafanua kuwa huduma ya Ultra Sound katika Mkoa wa Kigoma kwa sasa inapatikana katika Hospitali ya Mkoa ya Maweni na Hospitali Teule ya Batist kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wanaohitaji huduma hiyo.
Mhe. Senkamba amesema Serikali inatambua umuhimu wa kifaa cha Ultra Saund katika Vituo vya Afya vyote nchini na tayari imepeleka fedha Bohari ya dawa (MSD) kwa ajili ya ununuzi wa kifaa hicho ili kuhakikisha vituo vyote vinapokamilika vinakuwa na huduma ya Ultra Sound.
Aidha amesema ni azma ya Serikali kuhakikisha vituo vyote vya afya vinavyojengwa vikikamilika viweze kutoa huduma ya Ultra Sound, kuwa na wataalam wa kutosha pamoja na kuwa vifaa vya kutosha ili wananchi wapate huduma bora na kupunguza kero za afya katika jamii.
Na. Angela Msimbira BUNGE -DODOMA
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.