Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 29.9 kwa ajili ya kumalizia maboma yapatayo 2,392 nchini kote ili kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu kuingia kidato cha kwanza mwaka huu wanaanza masomo mara moja kabla ya kumalizika mwezi machi, 2019.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga katika Manispaa ya Musoma jana wakati akiongea na watumishi wa ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Kamati tendaji za Halmashauri ya Manispaa Musoma na Halmashauri ya wilaya Musoma baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi katika halmashauri hizo hii leo.
“katika kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza na hawakupata nafasi hapa nchini mwaka 2019, Serikali ya Daktari John Pombe Joseph Magufuli imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 29.9 ili kujenga maboma 2,392 ambapo wataweza kuendelea na masomo yao” alisema Nyamhanga.
Mhandisi Nyamhanga amesema kuwa wanafunzi wapatao 133,737 hawakupata nafasi kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu wa 2019 na ndio Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameamua kutolewa kwa fedha hizo kumaliza tatizo hilo.
Nyamhanga amesisitiza watendaji wote wa mikoa kusimamia fedha hizo na kwamba tayari zimeingizwa katika akaunti za shule husika zenye maboma na hivyo ukamilishaji wa maboma hayo ni lazima uwe wa muda mfupi ili wanafunzi waanze kuanza masomo yao mapema iwezekanavyo. Amesema maboma hayo lazima yakamilike kabla ya kumalizika mwezi machi, 2019 kama ilivyopangwa.
“Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa shule, Bodi za shule na kamati lazima zisimamie fedha hizo, mimi na ofisi yangu tutapita shule hadi shule na kuhakikisha kama fedha zilizopelekwa zimetuka kwa malengo yaliyokusudiwa” alisema Nyamhanga.
Imeandikwa Na: Fred Kibano
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.