Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga amewaagiza viongozi na wataalamu wanaotekeleza miradi mbalimbali Wilayani Hanang kukamilisha miradi viporo ya maendeleo kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha wa Serikali.
Ameyasema hayo leo Machi 03, 2024 wakati akikagua miradi ya Elimu katika kata ya Endasak na kituo cha Afya katika kata ya Nangwa kwenye ziara yake ya siku moja wilayani humo. RC Sendiga amesema ujenzi wa shule ya sekondari ya Chief Sarja ambao ni mradi wa muda mrefu umegharimu jumla ya shilingi Milioni 600 kujenga madarasa na nyumba za walimu lakini ujenzi huo haujakamilika hadi sasa.
Mhe. Mkuu wa mkoa amewataka viongozi wa kisiasa kusikiliza ushauri wa wataalamu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali badala ya kupingana nao na pia amewaagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi wa matumizi ya fedha za utekelezaji katika mradi wa shule ya Sekondari ya Chief Sarja.
Vilevile Mhe. Sendiga baada ya kutembelea mradi wa soko jipya lililojengwa baada ya lile la awali kuathiriwa na mafuriko mwishoni mwa mwaka 2023, amewaagiza viongozi wa Wilaya ya Hanang kuwa soko hilo lianze kutumika mara moja na wafanyabiashara katika wilayani humo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amewaagiza TARURA kufanya marekebisho katika maeneo ya soko hilo ikiwemo kujenga mitaro ya pembezoni mwa soko pamoja na ukarabati wa maeneo madogo madogo sokoni hapo ili biashara zianze kufanyika katika eneo hilo.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.