Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mh.Alexander Mnyeti amewataka wakala wa Barabara Taifa (TANROADS) Mkoani Manyara kuanza mchakato wa kuweka taa za barabarani katika Barabara kuu iendayo Dodoma na Arusha katika kipande kuanzia makutano ya barabara ya Singida (CCM Mkoa) hadi kona ya kwenda Mrara kwani kipande hicho kinakuwa na giza kipindi cha usiku na wavuka barabara wengi sana.
Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo alipokuwa katika mkutano wa Bodi ya Barabara Mkoani Manyara uliowakutanisha wadau wote wa Mkoa ikiwemo Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri,Wabunge, na wadau kutoka taasisi mbalimbali uliofanyika katika jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
“Tanroads wekeni taa za barabarani pale kuanzia CCM Mkoa dadi kona ya Mrara na kwenye vivuko vyote wa watembea kwa miguu ili tuepuke ajali maana magari katika eneo lile yakwenda kwa kasi mno” Alisema Mh.Mkuu wa Mkoa.
Akitoa ufafanuzi juu ya uwekwaji wa taa katika eneo hilo Meneja wa Tanroads Mkoa wa Manyara Mhandisi Bashiri Rwesingisa alisema kuwa tayari wameagiza taa za barabarani na muda si mrefu taa hizo zitafungwa ili kuepukana na ajali na vibaka hasa kipindi cha usiku.
Wakichangia mada wajumbe waliohudhuria kikao hicho walisifia Tanroads na TARURA kwa kuweka miundo mbinu ya barabara vizuri hasa katika Halmashauri ya Mji wa Babati kwani karibu barabara zote zinapitika katika kipindi chote.
(Kwa picha mbalimbali na Video angalia sehemu ya Kituo cha Habari kisha nenda Maktaba ya Picha na Maktaba ya Video)
Imeandikwa Na: Haji A. Msovu
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.