Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mh.Alexander Mnyeti amewataka wafanyakazi wote waliopo Mkoani Manyara kufanya kazi kwa bidii ili kutatua kero za wananchi Mkoani Manyara.
Mh.Mnyeti aliyasema hayo alipokuwa akiongea na wakuu wa Idara na Vitengo kutoka katika Halmashauri zote saba zilizopo Mkoani Manyara katika kikao kazi kilichofanyika kuanzia tarehe 18 hadi 19 Oktoba 2018 Mirereani Wilayani Simanjiro.
"Kupitia kikao hiki nawataka wafanyakazi wote wa Mkoa wa Manyara kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wananchi wanatatuliwa kero zao kwa wakati na bila usumbufu wa aina yoyote" Alisisitiza Mh.Mnyeti.
Vilevile aliwaagiza wakurugenzi wa Halmashauri zote zilizomo Mkoani Manyara kuhakikisha wanakusanya mapatao ya Halmashauri kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato vilivyomo katika Halmashauri zao.
Pia alimuagiza Mpima Ardhi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kupita kwenye Halmashauri zote ili kuhakikisha mipaka ya Mkoa wa Manyara inajulikana ili kuepusha migogoro ya mipaka kati ya Mkoa wa Manyara na Mikoa ya jirani.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara ameanzisha utaratibu wa kukutana na Wakuu wa Idara na Vitengo wote kutoka Halmashauri saba zilizopo Mkoani Manyara kila baada ya miezi mitatu ili kujadiliana juu ya mambo mbalimbali kuhusu maendeleo na changamoto mbalimbali na namna ya kuzitatua.
(Kwa picha mbalimbali angalia sehemu ya Kituo cha Habari kisha nenda Maktaba ya Picha)
Imeandikwa na: Haji A.Msovu (Afisa Habari Mkoa wa Manyara)
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.