Mkuu wa Mkoa wa Manyara joseph Mkirikiti amewata watanzania kutoruhusu watu wenye nia mbaya ya kuwagawanya watanzania kisiasa katika kipindi hiki cha maombolezo kufatia kifo cha aliyekuwa Rais wa jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Joseph Magufuli.
Alisema hayo wakati akitoa salam za rambi rambi kufatia kifo cha aliyekuwa Rais wa jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kilichotokea jana ambapo alieleza kuwa ni wakati wa watanzania kuhakikisha wanaendeleza amani ambayo tayari ilishakuwepo na kuwa sehemu ya kudumisha ulinzi na usalama.
"Lakini tukumbuke kama Mkoa na kama Taifa wapo watu inawezekana hawakuwa na nia nzuri na Taifa letu huu ni muda wa kuwa na umoja zaidi,tuwabaini na tuhakikishe kabisa hatuwapi nafasi ya kutugawanya watanzania na kama wanamanyara zaidi sana katika kipindi cha maombolezo tunawahakikishia wananchi wa Manyara Mkoa wetu ulinzi na amani itaendelea kudumishwa"Alisema Mhe. Mkirikiti.
Alisema wale wote wenye nia mbaya endapo itabainika Mtu mmoja mmoja au kikundi cha watu wanazusha jambo ni vizuri wananchi wenye nia njema kutoa taarifa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama ili waweze kuhakikisha maadui ambao wanania mbaya na taifa hili hawapati nafasi.
Mkirikiti akawaomba viongozi wa dini zote kuendelea kumwombea aliyekuwa Rais wa Tanzania Marehem John Joseph Magufuli na kuendelea kuwa ni vyombo vya kudumisha amani ikiwa ni pamoja na kutoa mafundisho kwa waumini wao yale ambayo yanawafanya watanzania kuwa na umoja zaidi na siyo vinginevyo.
Aliwataka vijana pia kutokupokea kila taarifa na kuzisambaza kwani wanatakiwa kupokea taarifa ambazo zitatoka kwenye mamlaka husika za serikali,hivyo wasikubali kupokea maneno ya uzushi ambayo yanapenyezwa na watu ambao hawaitakii mema nchi yetu.
"Niwaombe wanasiasa huu ni muda wa kuwa pamoja zaidi kuliko kuwa ni watu ambao tunagawanyika" Aliongeza.
Pia akawataka watumishi wote wa serikali kuendelea kuhakikisha wanatoa huduma kwa jamii ikiwa ni maji,umeme na afya huku akisisitiza kuwa tayari kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wameshakutana kwa dharura na wamejipanga vyema kuhakikisha kila jambo linasimamiwa kama inavyotakiwa.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.