Mamlaka ya anga Tanzania imeanza mchakato wa ujenzi wa Uwanja wa ndege uliopo Kata ya Mwada Kijiji cha Mbuyuni Mkoani Manyara.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Bwana Musa Missaile alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya uwepo wa uwanja wa ndege Mkoani hapo kwenye kikao cha Bodi ya barabara kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa.
Alisema kuwa kwa sasa Mkoa umeshapata eneo linakidhi vigezo kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege.
“Tumeshatembelea eneo hilo na kuna sehemu ya eneo limeenda hadi kwenye makazi ya wananchi kaya zaidi ya 80 na tumekubaliana nao kwasababu kuna eneo limebaki kubwa kwa upande wa chini ambalo ni eneo la serikali,walikuja wakalikagua wakaona wanaweza kulibadilisha kuwa eneo la makazi ili waweze kupisha ujenzi ufanyike kwa haraka na wananchi wamekubali kupisha ujenzi huo”alisema Missaile.
Alisema kukubali kwa wananchi hao kumepelekea wepesi kwa mamlaka ya hali ya anga ambapo mpaka sasa mamlaka hiyo imepeleka maombi hazina kwa bajeti ya 2022/23 ili kuanza ujenzi huo mapema na hivyo kurahisisha usafiri wa wakazi wa Mkoa wa Manyara na watalii wanaokuja kutembelea mbuga mbalimbali za wanyama kama Tarangire,Ziwa Manyara na Ngorogoro iliyo karibu na Mkoa wa Manyara.
Mkoa wa Manyara ni miongoni mwa Mikoa michache ambayo haikuwa na viwanja vya ndege tangu kuanzishwa kwake,kuanzishwa kwa uwanja huo kutarahisisha shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi Mkoani hapo.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.