Na, Ruth Kyelula, Manyara RS.
Wakulima Mkoani Manyara wametakiwa kuongeza thamani ya mazao ya mbogamboga na mikunde kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali zinazotokana na mazao hayo ili waweze kupata masoko ya uhakika ya ndani na nje ya nchi badala ya kuuza mazao ghafi kwa bei ya chini.
Akizungumza katika mafunzo ya kuongeza thamani ya mazao ya mbogamboga na mikunde Oktoba 10, 2025, yaliyoandaliwa na Shirika la World Vegetable Center kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara pamoja na SIDO, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Faraja Ngerageza amesema itasaidia kuongeza thamani ya mazao yanayopatikana ndani ya Mkoa wa Manyara.
Kwa upande wake mtafiti mwandamizi wa Kitengo cha Uchumi Jamii kutoka Shirika la World Vegetable Center, Inviolata Dominic,amesema mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wajasiriamali na wakulima wanaotengeneza bidhaa mbalimbali kutokana na mbogamboga na mikunde .
Meneja wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Manyara, Abel Mapunda amewataka wananchi kufika katika shirika hilo la kuhudumia viwanda vidogo, ili wajifunze ujasiriamali utakaowasaidia kuwainua kiuchumi.
Afisa Biashara wa Mkoa wa Manyara, Ally Mokiwa, amesema mafunzo hayo yatawasaidia wajasiriamali na wakulima kuinua kipato chao kupitia ubunifu.Aidha alisema kuwa anategemea baada ya kutoka kwenye mafunzo hayo watakuwa na uwezo mkubwa wa kutengeneza malighafi zao.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo ya usindikaji wa bidhaa za mboga mboga, wamesema mafunzo hayo yatawasaidia kiuchumi kwa kuongezewa thamani katika bidhaa zao na biashara zao.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.