Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Viijana, Kazi, Ajira na watu wenye ulemavu Mhe. Profesa Joyce Ndalichako amefanya ziara ya ukaguzi wa maandalizi ya kuelekea kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 kitakachofanyika Mkoani Manyara Oktoba 14.
Katika ziara hiyo, Mhe. Ndalichako amepokea taarifa ya maandalizi kwa ujumla kutoka kwa mratibu wa Mbio za Mwenge Mkoa Bw. Samwel Pastory katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Bw. Pastory ameeleza juu ya ukamilishaji wa uwanja wa Kwaraa na amemuhakikishia Waziri Ndalichako kuwa kamati zote zilizopangwa zimejipanga vizuri, pia ameeleza kuwa mafunzo kwa upande wa Watoto wa halaiki yanaendelea na sale za watoto hao zimesha wasili.
Aidha mratibu huyo amemueleza Mhe. Waziri kuwa uhamasishaji unaendelea kwa Halmashauri zote ikiwa ni pamoja na kuandaa bonanza kwaajili ya uhamasishaji mkubwa wa watu kujitokeza kwa wingi.
Vilevile Mhe. Ndalichako ametembelea uwanja wa kwaraa kuona mwenendo wa ujenzi unaoendelea katika uwanja huo. Mhe. Waziri amefurahishwa na kasi ya umaliziaji wa uwanja ikiwa ni pamoja na kuezekwa kwa mapaa katika majukwaa yote matatu, kukamilika kwa eneo la kukimbilia (running track) kwa kiwango cha rami, pia kukamilika kwa nyasi katika eneo la uwanja.
Katika ujio wake, vilevile ametembelea kanisa la Roho Mtakatifu ambako itafanyika Misa maalumu kwaajili ya kumbukizi ya Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere na amewataka wananchi wote wa Mkoa wa Manyara kwa ujumla kujitokeza siku ya kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Oktoba 14.
Aidha, Profesa Ndalichako amefanya ukaguzi katika eneo la uwanja wa Stendi ya zamani kutakapo fanyika maonesho ya wiki ya vijana kitaifa, ambapo amewataka vijana kujitokeza kwa wingi katika maonesho ya wiki ya vijana ili kuweza kujifunza na kupata ujuzi wa mambo mbalimbali yenye tija katika maisha yao na kuupongeza Mkoa wa Manyara kwa maandalizi mazuri.
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.