Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe.Joseph Mkirikiti amewaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri zilizopo Mkoani kwake kuhakikisha wanawapa mikopo waendesha bodaboda kutoka kwenye asilimia nne inayotengwa kutokana na mapato ya ndani kwa ajili ya vijana ili waweze kupata maendeleo.
Akiongea leo ofisini kwake na viongozi wa waendesha bodaboda kutoka Wilaya ya Babati Mhe.Mkuu wa Mkoa amewataka waendesha bodaboda Mkoani Manyara kutambua kuwa wanapaswa kuona kuwa hiyo ndio ajira yao inayoendesha Maisha yao na familia zao hivyo lazima wahakikishe wanajitambua na kujiweka kwenye vikundi ili waweze kupatitiwa mikopo na Halmashauri kwani wao ni sehemu ya vijana wanaotakiwa kunufaika na Mikoipo ya asilimia nne kutoka Halmashauri.
“Nataka bodaboda iwe kazi, Napataje nguvu ya kuyasema haya? Lazima niwalinde kwa sababu kuna watu waliwaahidi kuwanunulia bodaboda, huo sio mfumo mzuri, ili tutengeneze mfumo mzuri na mfumo mzuri ni hii asimia nne ya mapato ya Halmashauri hata bodaboda wakipata asilimia 0.1 itaenda kusaidia watu kumiliki Pikipiki zao badala ya kutegemea kuahidiwa bodaboda tatu, Bodaboda tatu zitawasaidia wapi lazima Mkurugenzi kwenye mapato yake ya ndani ajue bodaboda nao ni vijana?” Alisema Mhe.Mkirikiti.
Akizungumzia juu ya fedha za mfuko wa jimbo Mhe Mkuu wa Mkoa aliwataka Waheshimiwa Wabunge mara tu watakapochaguliwa wahakikishe wanatenga asilimia kadhaa kwa ajili ya bodaboda ili kuwasaidia vijana hao walioamua kujiajiri.
“Nataka nitangaze rasmi ndani ya Mkoa wangu kwamba Mbunge atakayechaguliwa ajue kuna bodaboda na awape asilimia na nna uhakika tukikuliana nchi nzima kila Mbunge achangie bodaboda kutoka kwenye fedha za mfuko wa jimbo itasaidia sana” Alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Wakati huohuo Mhe. Mkuu wa Mkoa amewataka waendesha bodaboda hao kupitia viongozi wao kujiwekea akiba kwa maendeleo yao ya badae kwani kazi hizo hawawezi kuzifanya milele.
“Nendeni kila mtu kwenye kijiwe chake angalieni ajenda ya jinsi ya kupata Mikopo na ile pesa itakuja kwa maana ya bodaboda wote sasa tumieni viongozi wenu ili mwende mbali Zaidi kufanya maendeleo kwa nguvu zenu wenyewe, bodaboda mna akili na mnaweza kujiongoza wenyewe” Alisema Mhe.Mkuu wa Mkoa.
Akiongea kwenyekikao hicho Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Manyara Bwana Joseph Michael amewapongeza waendesha bodaboda kwa kuwa na mfuko wao wa kuchangishana na kuwaahidi kuwaletea mtaalamu kwa ajili ya semina ya kujikwamua na kupata maendeleo yao na kuwataka waendesha bodaboda wote waende katika ofisi za LATRA kwa ajili ya kujipatia leseni kwa gharama ya shilingi elfu kumi na saba tu.
“Pamajo na bodaboda Wilaya ya Babati kuwa na viongozi wazuri lakini nawasisitizi juu ya kupunguza mwendo hasa kwenye makazi ya wat una kwenye vivuko vya watembea kwa miguu kwani sharia inatuelekeza ndani ya eneo la wazi usizidi spidi hamsini” Alisema Meneja wa LATRA.
Naye Mwenyekiti wa waendesha bodaboda Wilaya ya Babati Bwana Omari Adamu Bakari akimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa niaba ya waendesha bodaboda wote alisema kuwa wao binafsi wamefurahi kukutana na Mkuu wa Mkoa na wamemuahidi kuyafanyia kazi yale yote aliyoyasema.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kwa kweli tangu Mkoa huu umeanzishwa hatujawahi kupata heshma kama uliyotupa wewe ya kutuita na kukaa Pamoja ili kuzungumza mambo yanayotuhusu kwa utulivu na ufasa, ahsante san ana Mwenyezi Mungu akubariki” Alimalizia Bwana Omari
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.