Kampeni za upimaji virusi vya ukimwi kwa hiari zilizinduliwa rasmi tarehe 29/8/2018 katika wilaya ya Hanang mkoa wa Manyara. Kampeni hizo zililenga kuhamasisha, kuelimisha na juu ya upimaji wa VVU/UKIMWI, uzaziwa mpango na kifua kikuu na pia kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma bora za ili kufikia malengo ya kitaifa 90, 90, 90 ifikapo mwaka 2030.
(Baadhi ya wadau waliojitokeza katika kampeni ya Furaha Yangu-Pima,Jitambue, Ishi iliyozinduliwa kimkoa Wilayani Hanang 29 Augusti,2018.)
Akisoma taarifa ya mradi wa Taasisi inayoongozwa na Rais mstaafu wa awamu ya tatu Mh.Benjamin Mkapa (Benjamin Mkapa Foundation) Dkt Daud Isaya alisema taasisi yao inatekeleza mradi wa upimaji jumuishi wa VVU/UKIMWI na kifua kikuu na kuwaelimisha wananchi juu ya tabia hatarishi ziletazo maambukizi ya virusi na kuwahamisha wawe na tabia za kupima afya zao mara kwa mara. Taasisi yetu inatekeleza mradi huu kwa muda wa miaka 3 ambao umeanza June2018 hadi Disemba 2020,katika utekelezaji kwa Mkoa wa Manyara umeanza June katika Halmashauri mbili ambazo ni Simanjiro na Mbulu.
Katika Wilaya ya Hanang mradi huu ulianza tarehe 25 agosti na mpaka kufikia tarehe 28 mwezi huu jumla ya watu 1826 walijitokeza kupata huduma mbalimbali za kiafya kati yao wanaume 771 na wanawake 655 walipimwa kati yao watu 5 waligundulika kuwa na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi ambapo 3 ni wanaume na wa 2 ni wanawake wote waliunganishwa na huduma za matunzo na matibabu kwa vituo vya karibu.
(Baadhi ya wadau waliojitokeza katika kampeni ya Furaha Yangu-Pima,Jitambue, Ishi iliyozinduliwa kimkoa Wilayani Hanang 29 Augusti,2018.)
Vilevile uchunguzi wa awali wa kifua kikuu ulifanyika jumla ya watu 1422,walipimwa katiyao 33 walikutwa na dalili za kifua kikuu na kupewa rufaa kwenda hospitali ya Wilaya, upimaji wa shinikizo la damu jumla ya watu 1084 walipimwa kati yao 32 walikutwa na shinikizo la damu lisilo la kawaida na pia upimaji wa kiwango cha sukari jumla ya watu 102 walipimwa kati yao 7 walikutwa na kiwango cha sukari kisicho cha kawaida. Zoezi hili pia liliambatana na uchangiaji wa damu salama ambapo jumla ya chupa50 za damu zilikusanywa.
Huduma nyingine zilizotolewa ni uzazi wa mpango ikiwamo ugawaji wa kondomu ambapo jumla ya kondomu 4320 ziligawiwa, aidha elimu za ujasiriamali kutoka katika taasisi za kifedha kama NMB na CRDB zilikuwepo, elimu za mienendo ya tabia kupitia vikundi vya ngoma na sinema pia zilitolewa.
Aidha napenda kuishukuru serikali ya Tanzania na ya Mkoa wa Manyara kwa kushirikiana na taasisi yetu katika mradi huu na miradi mingine mingi iliyoanzishwa kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya.
(Mkuu wa Wilaya ya Hanang Mh.Joseph Mkirikiti akisalimiana Mratibu wa Mkapa Foundation Dkt.Daudi Isaya katika kampeni ya Furaha Yangu-Pima,Jitambue, Ishi iliyozinduliwa kimkoa Wilayani Hanang 29 Augusti,2018.)
Akitoa hotuba yake Mgeni rasmi katika sherehe hizo Mkuu wa Wilaya ya Hanang Mh.Joseph Mkirikiti alisema kuwa “bado idadi ya wanaume katika upimaji hairidhishi hivyo nawasihi waendelee kujitokeza kupima afya zao na pia kwa wanawake wasikate tama waje kupima na wazidi kuwaasa waume zao nao waje kupima afya zao” alisisitiza. Aidha aliwataka wananchi wawe na tabia za kwenda kupima afya zao na ili kufikia malengo ya 90, 90, 90 ni lazima kila mtu apime kwani mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI yanamhusu kila mtu katika jamii.
Vilevile alizitaka mamlaka zinazohusika na afya bora kutilia mkazo kampeni za uchimbaji wa Vyoo kupitia kauli mbiu isemayo “ Usichukulie poa Nyumba ni choo” ili kufikia malengo ya afya bora ni lazima kila kaya iwe na choo na pia kuhakikisha wanyama kama Mbwa wanafuungiwa kwani idadi yao imezidi kuwa kubwa na wanazagaa mitaani hivyo wanaweza kusababisha madhara kwa wananchi.
(Baadhi ya wadau waliojitokeza katika kampeni ya Furaha Yangu-Pima,Jitambue, Ishi iliyozinduliwa kimkoa Wilayani Hanang 29 Augusti,2018.)
Akimalizia hotuba yake alitoa shukrani kwa mashirika, wadau, taasisi na wananchi waliohudhuria kuifanikisha sherehe hiyo na pia aliishukuru serikali ya awamu ya tano kupitia ilani ya Chama Cha Mapinduzi inavyojikita katika mpango wa maendeleo na kuboresha miundo mbinu na vituo bora vya Afya, ambapo kauli mbiu ya mwaka huu 2018 ni “Furaha yangu- pima, jitambue, ishi”.
(Kwa Picha mbalimbali na video angalia Kituo cha Habari kisha nenda Maktaba ya Picha na Maktaba ya Video)
Imeandikwa na Isabela Joseph (UDSM-Mafunzo kwa Vitendo)
Copyright ©2022 Manyara Region Secretariet . All rights reserved.